NEWS

Thursday 8 October 2020

TCAA yahamasisha wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira sekta ya anga

Mkufunzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Thamarat Abeid akitoa mafunzo kuhusu sekta ya anga kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tarime leo.

 

MAMLAKA ya Anga Tanzania (TCAA) imehawamasisha wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira katika sekta ya anga ambayo inakua kwa kasi nchini.

 

Akizungumza wakati wa mafunzo kuhusu sekta ya anga kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tarime leo Oktoba 8, 2020, Mkufunzi Mkuu wa TCAA, Thamarat Abeid amesema sekta ya anga ina fursa lukuki za ajira kwa sasa.

 

“Ninaomba wanafunzi mjue kuwa hii ni bahati, kuna fursa katika sekta ya anga, msome kwa bidii muingie kufanya kazi sekta ya anga,” Abeid amewambia wanafunzi wa shule hiyo ya wavulana yenye kidato cha tano na sita.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tarime wakimsikiliza Mkufunzi Mkuu wa TCAA, Thamarat Abeid (hayupo pichani) wakati akiwaelimisha masuala yanayohusu sekta ya anga, leo.

 

Mbali ya kuajiriwa TCAA, Abeid ametaja nafasi za ajira zinazopatikana kwenye sekta ya anga kuwa ni pamoja na urubani, uhandisi au ufundi mitambo na uongpozaji wa ndege wakati wa kurua na kutua.

 

Ametaja fursa nyingine za ajira katika sekta hiyo kuwa ni kufanya kazi mbalimbali kwenye kampuni za ndege ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongoza na kuhudumia abiria wa ndege.

 

Kwa mantiki hiyo, amewataka wanafunzi kutoogopa masomo ya sayansi akisisitiza kuwa ili uwe rubani, mhandisi au fundi mitambo ya ndege lazima uwe umesoma masomo ya sayansi yakiwemo hesabu, fizikia na jiografia.

Mmmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tarime (aliyesimama) akiuliza swali kwa Mkufunzi Mkuu wa TCAA, Thamarat Abeid (hayupo pichani) aliyekwenda kuwafundisha masuala ya sekta ya anga shuleni hapo leo. (Picha zote na Peter Hezron)

 

Akijibu swali lililoulizwa na mwanafunzi kwamba kwanini asilimia 90 ya wanaosomea urubani lazima wajue hesabu, jiografia na kiingereza, Abeid amesema urubani unahitaji hesabu zaidi ndio maana wanalazimika kusoma somo hilo na kuhusu kiingereza amesema ni miongoni mwa lugha kuu zilizoidhinishwa na Shirika la Ndege la Kimataifa kutumika katika sekta ya anga.

 

Katika mafunzo hayo, wanafunzi wengi wameonesha nia na utayari wa kuchangamkia fursa za masomo katika chuo cha usafirishaji wa anga ili waweze kupata ajira TCAA na kwenye kampuni mbalimbali za ndege ndani na nje ya nchi.

 

Mbali ya mkoa wa Mara, Abeid amesema TCAA imeshatoa mafunzo kama hayo kwa wanafunzi wa shule za sekondari katika mikoa kadhaa nchini ikiwamo Tabora, Kagera, Mwanza, Simiyu na Kigoma.

 

Shule ya Sekondari ya Tarime ni miongoni mwa shule kongwe za serikali, ipo wilayani Tarime, Mara ambapo hupokea wavulana wa kidato cha tano na sita kutoka maeneo mbalimbali nchini.

 

(Imeandikwa na Lilian Tesha, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages