NEWS

Wednesday 7 October 2020

Waitara amwaga ahadi kemkem Tarime Vijijini

Mgombea ubunge jimbo la Tarime kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (wa pili kulia) akihutubia mkutano wake wa kampeni katani Nyanungu jana. Wa kwanza kulia ni mgombea udiwani wa kata hiyo, Tiboche Richard.


MGOMBEA Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwita Waitara ameahidi kwamba akichaguliwa atahakikisha anarejesha uhusiano baina ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na wakazi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo jimboni humo.

Wakazi wa kata ya Nyanungu wakimsikiliza mgombea ubunge katika jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) kijijini Kegonga leo. 

 
Akijinadi katika mkutano wa kampeni katika kijiji cha Kegonga leo Oktoba 7, 2020, Waitara amesema kero za wanavijiji kukamatwa na kunyang’anywa mifugo ndani ya hifadhi hiyo zitabaki historia kwani atashawishi mamlaka husika kuwaongezea maeneo yatakayokidhi mahitaji ya malisho ya mifugo yao.

 Kwa upande mwingine, mgombea huyo ameahidi kutumia nafasi ya ubunge kuhakikisha kijiji cha Kegonga kinajengewa shule ya sekondari na kuunganishiwa huduma ya umeme.

Mamia ya wananchi wakimshangilia kwa bashasha mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) katika mkutano wa kampeni kijijini Nyabichune, Matongo leo.

 

Pia Waitara amesema atahakikisha umeme unaunganishwa katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo kikiwamo kijiji cha Masanga ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

 

Waitara ametaja vipaumbele vyake vingine kuwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za afya, maji na barabara zinaboreshwa kwa kiwango cha kuridhisha katika maeneo yote ya jimbo la Tarime Vijijini sambamba na utoaji mikopo ya mitaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.

Wananchi walivyofurika kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) kijijini Nyabichune, Matongo leo. (Picha zote na Peter Hezron)

 
“Tumejipanga vizuri, ninawaomba Oktoba 28, 2020 msifanye kosa, nichangueni kuwa mbunge wenu, chagueni wagombea wenzangu wa CCM kwa nafasi za rais na madiwani, tumejipanga kuwatumikia,” amesema Waitara.

 Awali, kabla ya kwenda Nyanungu, Waitara amefanya mkutano wa kampeni katika kata ya Matongo ambako amesikiliza na kuahidi kutatua kero mbalimbali za wakazi wa vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo katani humo.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages