NEWS

Sunday 4 October 2020

Waitara aahidi kununua tingatinga Tarime Vijijini

 

Mwita Waitara (katikati) akipiga makofi na kufurahia ngoma ya asili (haipo pichani) wakati ikitumbuiza kwenye mkutano wake wa kampeni za ubunge uliofanyika katani Nyanungu, jimbo la Tarime Vijijini, leo. (Picha na Peter Hezron)

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwita Waitara, amesema akichaguliwa atahakikisha grader (tingatinga) linanunuliwa kwa ajili ya kulima barabara za vijiji na vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

“Tutanunua grader ya halmashauri ili wenyeviti wa vijiji wawe wanaomba wanawekewa mafuta wanasimamia inalima barabara za vitongo na vijiji, tutaimarisha barabara zetu,” amesema Waitara.

Msanii wa ngoma ya asili ya Kikurya akitumbuiza katika mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) uliofanyika katani Nyanungu, leo. (Picha na Peter Hezron)

Pia mgombea huyo ameahidi kuishawishi serikali kununua mtambo wa kuchimba visima vya maji katika taasisi za umma zikiwemo shule, zahanati na vituo vya afya ili kuboresha huduma za taasisi hizo.

Aidha, Waitara amesema akipata ridhaa ya wananchi ya kuwa mbunge, atahakikisha kuwa Shule ya Sekondari ya Nyanungu inapandishwa hadhi ya kuwa na kidato cha tano hadi sita kuanzia mwakani, na kwa upande wa umeme amesema ataweka msukumo ili vijiji vya kata hiyo vikiwamo Kegonga na Nyandage vinafikiwa na huduma hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu (2020).

Mamia ya wananchi wakimsikiliza mgombea ubunge jimbo la Tarime kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) akijinadi kwao katika mkutano wa kampeni uliofanyika katani Nyanungu, leo. (Picha na Peter Hezron)

Kwa upande mwingine, ameahidi kutumia fedha za mfuko wake kugharimia ujenzi wa choo cha wanafunzi katika Shule ya Msingi Masanga ya jimboni humo.

“Niungeni mkono kwa kunichagua kuwa mbunge wenu, mengine yote tutayatatua bila kelele, kina mama watapata mikopo na wananchi wote maskini, hasa wazee watanufaika na fedha za TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania),” ameongeza.

Wazee maarufu wakiwamo wa kimila ni miongoni mwa mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) katani Nyanungu, leo. (Picha na Peter Hezron)

Waitara ametumia nafasi hiyo pia kuwaombea kura wagombea wenzake wa CCM, Dkt John Magufuli kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tiboche Richard kwa udiwani wa kata ya Nyanungu akisema “Chagua Tiboche, chagua Waitara, chagua Magufuli kwa maendeleo ya kweli.”

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages