WADAU wa usimamizi wa rasilimali za maji katika dakio la Mara-Mori wametakiwa kuweka mikakati thabiti ya kukabili uchafuzi na mabadiliko ya tabianchi katika dakio hilo kwa uendelevu na ustawi wa watu, wanyama na viumbe hai wengine.
Msisitizo huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Mtemi Msafiri, katika ufunguzi wa warsha ya jukwaa la wadau wa sekta mtambuka juu ya usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji na mabadiliko ya tabianchi katika dakio la Mara-Mori.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa, akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Warsha hiyo ya siku mbili imeanza jana Novemba 5, 2020 mjini Tarime chini ya uratibu wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria kwa ufadhili wa taasisi ya Vi Agroforestry kupitia Mradi wa SEMA (Serengeti – Mara Ecosystem Project).
“Ninawapongeza Vi Agroforestry kupitia Mradi wa SEMA kwa ufadhili wa mafunzo haya ambayo tunaamini yataongeza uelewa zaidi na mwelekeo sahihi juu ya utunzaji wa rasilimali za maji maana maji ni kila kitu,” amesema Marwa.
Aidha, amewataka wadau hao kufuatilia kwa makini na kuzingatia mafunzo hayo ili baadaye wayafanyie kazi kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuimarisha mipango ya kudhibiti uchaguzi wa maji katika dakio la Mara-Mori.
Wadau wa usimamizi wa rasilimali za maji katika Dakio la Mara-Mori wakishiriki warsha hiyo.
Awali, Katibu wa Jukwaa hilo, Mhandisi Mwita Mataro ambaye ni Afisa wa Maji Dakio la Mara-Mori, amesema mafunzo hayo pia yatawaongezea washiriki uwezo wa kujua wajibu wao katika utunzaji wa rasilimali za maji katika dakio hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Majura Maingu, amesema usimamizi thabiti wa rasilimali za maji katika Dakio la Mara-Mori utawezesha matumizi yake kuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi waBodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Jackline Jaco (aliyesimama), akizungumza katika warsha hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Jackline Jacob, amesema kila mdau ana jukumu la kudhibiti uchafuzi wa maji ukiwemo unaosababishwa na shughuli za uchimbaji madini, kilomo na ufugaji holela.
Mratibu wa SEMA Project, Amani Shipella, amesema mradi huo chini ya Vi Agroforestry wanatamani kuendelea kusaidia wakulima wadogo katika kilimo mseto na matumizi endelevu ya ardhi katika Dakio la Mara-Mori, hasa katika vikundi.
Pia kusaidia vikundi vya kupambana na wanyamapori waharibifu wa mazao, vikundi vya kufuga nyuki na uendelevu wa vikundi vya kujiingizia kipato.
“Lengo ni kusaidia katika uhifadhi wa mfumo ikolojia wa Serengeti – Mara na jamii za wakulima wadogo waliopo pembezoni mwa mfumo ikolojia huu,” amesema Shipella.
Mratibu wa SEMA Project, Amani Shipella, akiwasilisha mada katika warsha hiyo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Willie Mwaruvanda, amesisitiza kuwa ubora wa maji ni muhimu kwa ajili ya watu na shughuli zao, mimea, wanyama na viumbe hai wengine wote.
Mmoja wa washiriki, Regina Waryana (aliyesimama), akichangia mada katika warsha hiyo.
Washiriki wa warsha hiyo pia wamewezeshwa mada kuhusu umuhimu wa Bonde la Mto Mara kwa uhifadhi endelevu wa ikolojia ya Serengeti iliyowasilishwa na mtafiti wa wanyamapori, Emmanuel Masenga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
(Habari na picha zote na Mara Online News)
Kwa pamoja tunaweza kutunza rasilimali ya Maji
ReplyDelete