NEWS

Wednesday 16 December 2020

Joyce Mang’o apongeza uzinduzi wa Mara Online News

Joyce Ryoba Mang'o

 

ALIYEKUWA mtia nia ya ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joyce Ryoba Mang’o, amepongeza na kujivunia uanzishwaji na uzinduzi wa chombo cha habari cha kidijitali, yaani Blogu ya Mara Online News, akisema mkoa wa Mara umepata chombo cha kutangaza fursa lukuki za kiuchumi na uwekezaji zilizopo mkoani humo.

 

Mang’o ambaye pia alikuwa Meneja Kampeni za Ubunge Jimbo la Tarime Mjini zilizomwezesha Michael Kembaki (CCM) kuibuka mshindi wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 28, 2020, amesema mkoa wa Mara una rasilimali nyingi ambazo zikitangazwa na kutumika vizuri zitauwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo yanayogusa jamii nzima.

 

Ametoa pongezi hizo siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Kighoma Malima na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete kuzindua Blogu ya Mara Online News mjini Tarime katika viwanja vya ofisi za Taasisi ya Mara Online inayomiliki blogu hiyo na Gazeti la Sauti ya Mara linalotoka kila Jumatatu.   

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (mwenye kofia katikati), Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga (kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa pili kusshoto), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote (wa tatu kushoto), Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete (kulia), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mara Online, Jacob Mugini (wa pili kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Ghati wakipiga makofi na kushangilia baada ya mtoto Angel Jacob Mugini kukata utepe wa uzinduzi wa Blogu ya Mara Online News mjini Tarime, jana Desemba 15, 2020.

 

“Haya ndio maendeleo tunayoyataka. Mara tumepata pa kusemea mazuri yetu. Napenda kuipongeza Mara Online kwa uthubutu mkubwa wa kuzindua chombo cha kidijitali. Mara Online haitasaidia tu Mara bali Tanzania kwa ujumla.

 

“Rai yangu kwao ni kuwa ijikite zaidi kwenye kuitangaza Mara na utajiri wake, kuibua mambo makubwa yanayoweza kuipeleka Mara mbele ili kuvutia wawekezaji katika mkoa wetu.

 

“Zipo rasilimali nyingi katika mkoa huu ambazo bado hazijatumika vizuri kwa maendeleo endelevu ya Mara na Tanzania.

 

“Mara Online tunaitegemea kutoa elimu itakayosaidia watu wa Mara kuona fursa zinazowazunguka kwa maendeleo endelevu yanayogusa makundi yote ya jamii, yaani vijana, wazee, watoto na wanawake,” amesema Mang’o katika salamu zake za pongezi.

Joyce Ryoba Mang'o (katikati) akiwa na makada wenzake wa CCM katika mojawapo ya mikutano ya kampeni za ubunge jimbo la Tarime Mjini.

 

Mang'o ametumia nafasi hiyo ya pongezi pia kutoa wito kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Mara kuunga mkono juhudi za Mara Online katika kutangaza na kuelimisha umma fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo mkoani humo kwa manufaa ya wana-Mara na Taifa kwa ujumla.

 

Chombo cha habari cha kidijitali cha Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara vimeweka kipaumbale katika kuandika na kutangaza habari bora za maendeleo na uhifadhi wa wanyamapori, vyanzo vya maji ukiwemo Mto Mara na ikolojia ya Mara kwa ujumla.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

1 comment:

  1. Kongole Mara Online

    Mmekuwa chombo cha habari cha kizalendo ndani ya Mkoa wa Mara na nje ya Mkoa wetu.

    Yapo mambo makubwa naya msingi mnaweza kuya address na kuufanya Mkoa wetu na Wilaya yetu ya Tarime kuwa sehemu mbadala ya uzalishaji na uwekezaji.

    Andikeni habari za uwekezaji ndani ya Wilaya yetu na Mkoa,andikeni habari njema zihusuzo tamaduni njema za jamii yetu,andikeni habari zinazo elimisha madhara ya vita za koo na ukabila usio na tija....bila kusahau habari za utekelezaji wa ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI.

    Tunapaswa kuwa Mkoa wa mfano: kwenye agenda ya maendeleo,Mkoa wa mfano kwa watu wake kuwa na huduma bora na stahiki za Afya, Elimu na miundombinu mbalimbali inayochagiza uchumi.

    Tuwasaidie viongozi wetu kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi na si kuwa chombo cha habari kinachoongoza kuuchafua Mkoa wetu.

    Naendelea kuwapongeza sana kwa hatua hii kubwa.

    Asante.

    Nicodemus Keraryo

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages