
Na Mwandishi Wetu
Serengeti
--------------

Sehemu ya wajumbe mkutanoni

Dkt. Haule akihutubia mkutano huo


Serengeti
--------------
Wilaya za Serengeti, Rorya na Tarime mkoani Mara zimevuna tumbaku yenye uzito wa kilo milioni 3.84 katika msimu wa 2025/2026, huku Serengeti pekee ikizalisha kilo milioni 3.38.
Mgeni ramsi Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfan Haule, ameyasema hayo wilayani Serengeti leo Ijumaa katika mkutano wa vyama wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) vinavyolima tumbaku.
Dkt. Haule amesema mavuno ya zao hilo katika msimu huo wa 2025/2026 yameongezeka ukilinganisha na kilo milioni 2.65 zilizozalishwa msimu wa 2024/2025.

Sehemu ya wajumbe mkutanoni
“Uzalishaji mkubwa umechangiwa na wenzetu wa Serengeti, hatukufikia lengo la kuzalisha kilo milioni nne lakini walau tumepata hizo, na mipango yetu ni kuendelea kuongeza uzalishaji tufikie kilo milioni tano msimu huu wa 2026/2027,” amesema Dkt. Haule.
Ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa uzalishaji huo umechangiwa kwa kiwango kikubwa na mkopo wa pembejeo, hasa mbegu na mbolea kutoka serikalini.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwezesha kupata mkopo karibu Dola za Marekani milioni 1.363 msimu uliopita,” amesema Dkt. Haule.
Aidha, amesema mavuno ya tumbaku yaliyopatikana hayakunufaisha wakulima pekee, bali pia vyama vya msingi vya ushirika, WAMACU Ltd na halmashauri za wilaya hizo ambazo zimepata ushuru wa Dola za Marekani 468,450.

Dkt. Haule akihutubia mkutano huo
Dkt. Haule amehitimisha hotuba yake kwa kuelekeza ushirika wa WAMACU kusimamia miongozo ya kilimo cha tumbaku na kuendelea kuhamasisha uzalishaji mkubwa wa zao hilo la biashara ili kuinua mavuno na kipato cha wakulima.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia ubora wa zao la tumbaku kuanzia shambani hadi sokoni ili kuwezesha wakulima kupata bei nzuri na ulipaji wa mikopo ya pembejeo za kilimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco Lubela, amesema mavuno ya kilo milioni 3.38 za tumbaku yameiwezesha halmashauri ya wilaya hiyo kupata ushuru wa Dola 186,000 huku vyama vya msingi vya ushirika vilivyopo vikipata Dola 281,000 sawa na jumla ya shilingi milioni 600.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewakumbusha wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya usalama kudhibiti utoroshaji wa tumbaku kwenda nje ya nchi.

DC Angelina akizungumza katika mkutano huo
Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, amesema ushirika huo umeandaa mkutano huo kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa maelekezo na miongozo ya serikali sambamba na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa tumbaku katika msimu wa 2026/2027.

GM Gisiboye akisoma risala katika mkutano huo. (Picha zote na Mara Online News)
Tumbaku ni moja ya mazao muhimu ya biashara yanayoingiza fedha za kigeni kwa maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment