NEWS

Tuesday 5 January 2021

Waziri Aweso atoa maagizo kwa RUWASA

 

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa tatu kulia) akikagua mradi wa maji wa kijiji cha Gamasara wilayani Tarime, Mara leo Januari 5, 2021.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, leo Januari 5, 2021 amekagua mradi wa maji wa kijijini Gamasara uliopo nje kidogo ya mji wa Tarime mkoani Mara na kutoa maagizo kwa Wakala wa Huduma ya  Maji  na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wananchi wanaozunguka mradi huo wanapata huduma ya maji.

"Tutumie utaalamu wetu kuwawezesha wananachi kupata huduma ya maji," amesema Waziri Aweso.

Waziri Aweso (katikati) akisikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu mradi wa maji wa Gamasara.

Wanakijiji waliokuwa katika eneo hilo walimwambia Waziri Aweso kuwa  huduma ya maji katika mradi huo ambao umegharimu serikali mamilioni ya fedha inasuasua (siyo ya kuridhisha).

"Maji hayatoki muda wote, na huduma ya maji haipatikani kila siku," amesema mmoja wa wananchi hao na kushangiliwa na wenzake.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara (wa pili kulia) ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon (kushoto) ni miongoni mwa viongozi waliofuatana na Waziri Aweso katika ziara yake ya kukagua miradi ya maji ambayo inasimamiwa na RUWASA wilayani humo. 

Mbali na Gamasara, ratiba ambayo Mara Online News inayo inaonesha kuwa Waziri Aweso atakagua miradi ya maji mingine ya Magoma, Nyantira na Nyarwana wilayani Tarime.

Kesho Januari 6, 2021 Waziri huyo ataendelea na ziara ya kukagua miradi ya maji katika wilaya ya Rorya.

(Habari na picha na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages