KAMPUNI ya Gimmy Inter Co. Ltd yenye makao makuu jijini Dodoma, leo Januari 15, 2021 imetoa misaada mbalimbali yenye thamani ya Sh milioni 14.85 kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya elimu wilayani Serengeti, Mara.
Misaada hiyo ni pamoja na madawati 30 na viti vyake - vyote vyenye thamani ya Sh milioni 2.4, saruji mifuko 100 (Sh milioni 2.2), fedha taslimu Sh milioni 1.25 za kununua mabati 50 na eneo la ukubwa wa ekari tatu lenye thamani ya Sh milioni tisa kwa ajili ya upanuzi wa Shule ya Msingi Nyamerama.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gimmy Co. Ltd, Gimmy James Mgaya amewakilishwa na Diwani wa Kata ya Geitasamo, Joshua Nyansiri ambaye amekabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Diwani Nyansiri amesema Gimmy ametoa misaada hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Madawati 30 na viti vyake - vilivyotolewa msaada na mdau wa maendeleo, Gimmy James Mgaya kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Serengeti. |
Mkuu wa Wilaya, Babu, amemshukuru Mkurugenzi huyo wa Gimmy Co. Ltd kutokana na misaada hiyo na kutumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kujitokeza kuchangia maendeleo ya elimu wilayani Serengeti.
Naye Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Serengeti, Mwalimu Simon Mdaki amewataka wakuu wa shule zilizolengwa na misaada hiyo kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Baada ya hapo, Babu amekabidhi misaada hiyo kwa maofisa watendaji wa kata za Geitasamo, Machochwe, Mosongo, Nyambureti na Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kuigawa kwenye shule husika.
(Habari na picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment