NEWS

Thursday 28 January 2021

Polisi Tarime wanasa shehena ya bangi, watuhumiwa watatu


Sehemu ya magunia yenye bangi yaliokamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Tarime, leo Januari 28, 2021.

JESHI la Polisi katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara limekamata shehena ya magunia 80 yenye bangi na watu watatu waliokuwa kwenye lori lililokuwa likisafirisha zao hilo haramu kwenda jijini Dar es Salaam.


Ukamataji huo umefanyika leo Januari 28, 2021 katika kijiji cha Gamasara, ndani ya lori lenye namba za usajili T 465 DQJ na tela lenye namba T 143 DEM.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Tarime – Rorya, William Mkonda (katikati mbele) akizungumzia tukio la ukamataji wa magunia 80 ya bangi na watuhumiwa watatu leo Januari 28, 2021.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Tarime – Rorya, William Mkonda amewataja watuhumiwa waliokamatwa pamoja na bangi hiyo kuwa ni dereva wa lori hilo, Salum Issa (26) mkazi wa Nzega mkoani Tabora, kondakta wa lori hilo, Khalid Yusuf (44) mkazi wa jijini Mwanza na Amos Chacha (29) mkazi wa mjini Tarime.

Kamanda Mkonda akionesha wanahabari (hawapo pichani) magunia 80 yenye bangi yaliyokamatwa.

“Tunaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine kuhusiana na tukio hili la uhalifu na hawa tuliowakamata tunaendelea kuwashikilia huku tukiendelea na taratibu za kuwafikisha mahakamani,” amesema Kamanda Mkonda.

 

Kuhusu magunia 80 yenye bangi, RPC huyo amesema katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake leo kwamba yalikuwa yamefunikwa na magunia 15 ya mahindi mabichi kwenye lori hilo.

 

Kufuatia ukamataji huo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri amewataka watu wote wenye mashamba ya bangi wilayani humo kujisalimisha haraka iwezekanavyo kabla ya kushukiwa na rungu la dola.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tarime, Apoo Castro Tindwa (kushoto) na viongozi wengine wakishuhudia magunia 80 yenye bangi yaliyokamatwa na Polisi Tarime.
 

“Ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu, wilaya ya Tarime tumejipanga kuhakikisha kuwa usalama uko sawa,” amesema DC huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo.

Kichwa cha lori lililokamatwa likisafirisha bangi hiyo kwenda Dar Es Salaam

Viongozi hao wamewashukuru wananchi wanaoendelea kuvipatia vyombo vya dola ushirikiano ukiwemo wa kufichua vitendo vya uhalifu na wahalifu katika jamii wilayani Tarime.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages