Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara, Jerome Kiwia |
IDARA ya ardhi mkoa wa Mara imesema katika kipindi hiki cha Januari 2021 itaanza kuwafikisha mahakamani wananchi waliokaidi kulipa kodi ya ardhi kwa mwaka 2019/2020.
Akizungumza na Mara Online News ofisini kwake leo Januari 11, 2021, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara, Jerome Kiwia amesema muda uliotolewa na unaotakiwa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria umemaluzuka na sasa taratibu nyingine zinaendelea.
Kiwia amesema idara ya ardhi mkoa wa Mara imekuwa ikitoa taarifa mara kwa mara juu ya kulipa kodi ya ardhi na umuhimu wa kodi hiyo lakini baadhi ya wananchi wamekaidi, hivyo hatua inayofuata ni kuwafikisha mahakamani.
Amesema katika kipindi cha Oktoba na Novemba 2020 baada ya utoaji wa taarifa, wapo wananchi waliojitokeza kulipa kodi ya ardhi yanayotumia.
Kamishna huyo amesema kodi ya ardhi ya kipindi cha mwaka 2019/2020 ilipaswa kuwa imelipwa kufikia Juni 2020, lakini pamoja na wananchi kuongezewa muda hadi Desemba mwaka huo bado wapo ambao hadi sasa hawajailipa.
“Tumekuwa tukitoa taarifa mara kwa mara ya kuwataka wananchi kulipa kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria kwenye maeneo wanayoyamiliki.
“Muda uliotolewa wa kulipia umemalizika na sasa unaandaliwa utaratibu wa wadaiwa wote kufikishwa mahakamani ili kuweza kupatikana kwa kodi ya serikali,” amesema Kiwia.
Amewataka wananchi wote wa maeneo yaliyopimwa lakini hawana hati kufika kwenye ofisi za maofisa watendaji wa kata na serikali za mitaa kuchukua fomu kwa ajili ya kulipia maeneo yao.
Kiwia amesema kwa mujibu wa sheria, wananchi wanaomiliki ardhi hata kama hawana hati wanapaswa kulipia na utaratibu wa kuipata ni wa muda wa wiki moja.
(Imeandikwa na Shomari Binda, Musoma)
No comments:
Post a Comment