NEWS

Tuesday 5 January 2021

Waziri Aweso atumbua majipu RUWASA Mara

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (kulia) akitoa tamko dhidi ya Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Sadick Chakka (kushoto nyuma) na mwenzake wa Wilaya ya Tarime, Marwa Murasa (kushoto mbele) ambao ameagiza wavuliwe madaraka kwa uzembe wa kushindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji. Wa tatu kushoto ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

WAZIRI wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwavua madaraka Meneja wa Wakala wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Sadick Chakka na mwenzake wa Wilaya ya Tarime, Marwa Murasa.

 

Sambamba na hilo, Waziri Aweso amemwagiza Katibu Mkuu huyo kuunda kamati itakayochunguza miradi ‘kichefuchefu’ ya maji mkoani Mara, hasa katika wilaya za Tarime na Rorya na hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya watakaothibitika kuichakachua na kuikwamisha.

 

Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo Januari 5, 2021 baada ya kukagua mradi wa maji wa Magoto na kubaini ubabaishaji mkubwa wa wataalamu wasimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion K. Samwel (katikati) akimweleza Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (kushoto) ubabaishaji uliofanyika katika mradi wa maji wa Magoto katani humo. Kulia ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Marwa Murasa ambaye Waziri Aweso ameagiza avuliwe madaraka hayo.

“Mkoa wa Mara umekuwa na ubabaishaji mkubwa wa miradi ya maji, tuna miradi kichefuchefu ambayo ndiyo inachafua taswira ya Wizara, faraja ya Wizara ya Maji ni kuona wananchi wanapata maji,” amesema Waziri Aweso na kuendelea:

 

“Bora kisingizio ingekuwa kwamba fedha hamna, tulileta shilingi zaidi ya bilioni nane mkoani Mara na kwenye akaunti hadi sasa mna shilingi bilioni 3.66, nani atakuelewa – una bilioni tatu halafu hakuna maji.”

 

Waziri huyo wa maji ameelezea kukerwa kwake na uzembe wa viongozi wa RUWASA Mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime walioshindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji kama ilivyokusudiwa licha ya serikali kuwapa Sh milioni zaidi ya 100 kwa ajili ya usimamizi wa miradi hiyo.

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (wa pili kulia) na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakitoka kukagua mradi wa maji wa Magoto katani Nyakonga. Katikati yao ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Marwa Murasa ambaye Waziri Aweso ameagiza avuliwe madaraka hayo kwa kushindwa kusimamia utekelezaji chanya wa miradi ya maji wilayani.

Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani Tarime iliyosomwa na Meneja wa RUWASA mbele ya Waziri Aweso, inaonesha kwamba utekelezaji wa miradi zaidi ya 10 umefikia kati ya asilimia 90 na 95 lakini haitoi maji.

 

Katika ziara yake hiyo, Waziri Aweso amempongeza Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kusimama kidete katika kudai ufumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi jimboni humo ikiwemo ya ukosefu wa maji safi.

 

“Ninampongeza Mbunge Waitara kwa kuguswa na matatizo ya watu, Mungu ambariki sana, lakini tutampa ushirikiano wananchi wa Tarime wapate maji,” amesema Aweso.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages