NEWS

Tuesday 16 February 2021

Mawakala wa forodha mipakani watakiwa kuzuia magendo

Afisa Mkuu wa Utafiti, Sera na Mipango, Happyson Nkya kutoka TRA akizungumza na mawakala wa forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Sirari, Tarime mkoani Mara.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka mawakala wa forodha mipakani kutokuwa mawakala wa biashara za magendo bali wafuate sheria na taratibu za forodha za kuingiza na kutoa mizigo nchini.

 

Hayo yamesemwa leo Februari 16, 2021 na Afisa Mkuu Utafiti, Sera na Mipango kutoka TRA, Happyson Nkya alipokuwa akizungumza na mawakala wa forodha katika mpaka wa Sirari uliopo wilaya ya Tarime mkoani Mara.

 

Nkya amesema mawakala ni kiungo muhimu kati ya TRA na walipakodi, hivyo wanatakiwa kutoa taarifa sahihi kwa wateja wao kuhusu taratibu na kanuni za kutumia mpaka rasmi ili kuwasaidia wasijihusishe na biashara za magendo kwani zinaweza kuwaingiza katika hasara ya kufilisiwa mali na chombo kitakachokamatwa na magendo.

 

 "Ninyi mawakala wa forodha mpakani ni kiungo muhimu sana kwetu na walipakodikodi, hivyo tunawaomba msiwe mawakala wa biashara za magendo hapa mpakani bali muwe mabalozi wa kuwaelekeza wateja wenu taratibu za kiforodha ili serikali ipate mapato," amesema Nkya.

Kikao cha maofisa wa TRA na mawakala wa forodha kikiendelea mpakani Sirari.

Kwa upande wao, mawakala wa forodha mpakani hapo wameeleza kufurahishwa na hatua ya TRA kukaa na kuzungumza nao na wameahidi kuwa mabalozi kwa kuwa suala la biashara za magendo linaathiri pia biashara zao.

 

 "Sisi tupo tayari kuwa mabalozi na kuwaelekeza wateja wenu taratibu za kiforodha kwa sababu wakipita kwenye mpaka rasmi ndipo na sisi tunafanya biashara zetu vizuri na serikali inapata mapato," amesema John Duro kutoka kampuni ya Sunrise Logistics.

 

Wakala mwingine, Sncoslaus Nyang'oko anayewakilisha kampuni ya E3, amesema suala la biashara ya magendo mpakani pia linazorotesha shughuli zao, hivyo watashirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa magendo yanakuwa siyo sehemu ya biashara zao na kuwaelekeza wateja wao kutumia mpaka rasmi wa Sirari.

 

“Mawakala wa forodha tunafanya shughuli zetu kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kiforodha hivyo hatuwezi kuwa sehemu ya kufanya biashara haramu za magendo, tunakubali kuwa mabalozi wa kuwaelekeza wateja wetu kutumia mpaka rasmi,” amesisitiza Nyang’oko.

 

Wakala wa forodha mpakani Sirari, Sncoslaus Nyang'oko kutoka kampuni ya E3 LTD akizungumza katika kikao hicho.


TRA imekuwa ikifanya mikutano na wadau mbalimbali mkoani Mara ili kutoa elimu kuhusu taratibu za kiforodha za kufuata wakati wa kuingiza na kutoa mizigo katika mpaka wa Sirari kwa lengo la kujenga uelewa wa matumizi ya mpaka rasmi na kukabiliana na biashara za magendo.

 

(Imeandikwa na Rachel Mkundai, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages