NEWS

Monday 29 March 2021

Ukatili dhidi ya mtoto Rorya: Mwanaume wa miaka 52 aoa mwanafunzi wa miaka 15

Ng'ombe
 

KATIKA tukio la kushangaza, mzee mwenye umri wa miaka 52 anaidaiwa kumuoa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Bugire iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.

 

Vyanzo vyetu vya uhakika kutoka Rorya vimeeleza hivi karibuni kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 ameolewa na mwanaume huyo mwaka jana (2020) akiwa darasa la sita.

 

“Ina maana Januari mwaka huu (2021) huyu mwanafunzi huyo angekuwa darasa la saba,” kimeeleza chanzo chetu kutoka serikalini.

 

Taarifa zaidi zilizoifikia Mara Online News zinasema mwanaume huyo ametiwa mbaroni hivi karibuni na msichana huyo amerejeshwa kwa wanafamilia.

 

“Mzee aliyehusika kumuoa huyo mwanafunzi amekamatwa pamoja na mzazi wa msichana - aliyepokea ng’ombe wawili kama mahari wamekamatwa,” kimesema chanzo chetu.

 

Taarifa hizo zinadai kuwa mwanafunzi huyo ameolewa kuwa mke wa tatu wa mwanaume huyo.

 

“Kwa sasa anahitaji msaada hata wa kisaikolojia,” amesema ofisa wa serikali wilayani Rorya.

 

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugire, Jackson Nyangubo amezungumza na Mara Online News na kuthibitisha tukio la kuolewa kwa mwanafunzi wake huyo.

 

“Ni kweli huyo msichana ni mwanfunzi wa shule yangu na watuhumiwa [muoaji na mzazi] tayari wametiwa mbaroni,” amesema Mwalimu Nyangubo.

 

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi TarimeRorya, William Mkonda kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo.

 

Habari hizi zimechapishwa pia kwenye gazeti la Sauti ya Mara la leo Jumatatu Machi 29, 2021.

 

(Habari: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages