NEWS

Tuesday 28 September 2021

AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe yahamasisha elimu bora kwa watoto wote




WAZAZI, walezi na watu wote katika jamii, wamehimizwa kutoa fursa sawa ya elimu bora kwa watoto wa kike na kiume, wakiwemo wenye ulemavu.

Hayo yameelezwa na Afisa Mradi kutoka Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebecca Bugota wakati wa tamasha la kuhamasisha utoaji elimu bora kwa watoto wote bila ubaguzi, lililofanyika jana katika Shule ya Msingi Gwitare iliyopo kata ya Nyamwaga, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Rebecca akizungumza wakati wa tamasha hilo.

"Elimu bora ni haki ya kila mtoto bila kujali jinsi na hali zao," Rebecca amesisitiza na kuongeza kuwa wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike na kiume wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa, kufuatilia maendeleo yao na kuhakikisha mazingira ya kujifunzia ni bora.

Rebecca (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakikabidhi kombe kwa mwakilishi wa washindi.

Aidha, Rebecca ameitaka jamii kushirikiana katika kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. "Jamii iwalinde watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili," amesisitiza.

Naye Mwalimu wa Michezo katika Shule ya Msingi Gwitare, Revina Yohana amewataka wazazi na walezi kutoficha watoto wenye ulemavu, badala yake wawapatie fursa ya kupata elimu bora kama watoto wengine katika jamii.

Kwa upande wao, wanafunzi walioshiriki katika tamasha hilo wameomba elimu ya kupinga ukatili iendelee kutolewa.

Wawakilishi wa timu zilizoshinda wakionesha makombe waliyozawadiwa.

Hata hivyo, Rebecca amesema jamii imepokea mradi wa uhamasishaji elimu bora kwa watoto kwa mwitikio mkubwa na kwamba mahudhurio ya watoto katika shule ambazo wanatekeleza mradi huo yameongezeka.

Revina na Mwenyekiti wa Kijiji cha Gwitare, Daud Elias wameishukuru AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kuelekeza mradi huo katika eneo hilo, wakisema utasaidia utoaji wa elimu bora kwa kila mtoto na kukomesha ukatili dhidi ya watoto.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages