NEWS

Monday 11 October 2021

RC Hapi alihakikishia Kanisa la Waadventista Wasabato ushirikiano, alipongeza kwa utoaji huduma za kijamii

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Salum Hapi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) katika shughuli za maendeleo, zikiwemo za utoaji huduma za kijamii kama vile elimu na afya.

RC Hapi ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kufunga mahubiri ya setelite, yaliyoandaliwa na SDA Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania na kufanyika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Jumamosi iliyopita.

RC Hapi Katibu (kushoto) akipokewa na Katibu Mkuu wa SDA Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Mchungaji David Makoye (kulia).

Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia itaendelea kutoa uhuru wa kuabudu na kuheshimu ibada za kanisa hilo, kwani limekuwa likitoa mchango mkubwa katika huduma mbalimbali za kijamii.

“Nawaletea salamu kutoka kwa Rais wetu, mzidi kumuombea. Pia nawapongeza namna kwa mnavyotoa elimu bora kwa watoto, maana kama hakuna familia bora hakuna taifa imara. Serikali itaendelea kuwaunga mkono Wasabato kwa huduma mbalimbali mnazotoa,” RC Hapi ameongeza.
RC Hapi amelipongeza kanisa hilo kwa kurusha mahubiri yanayohamasisha amani kwa lugha za Kiswahili, Kifaransa, Kiarabu, Kingereza na lugha ya alama kwa wenye ulemavu wa kusikia, yaliyorushwa kote duniani kutokea kanisa la SDA Kewanja Nyamongo.
Naye Katibu Mkuu Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Mchungaji David Makoye amesema kanisa hilo lina waumini zaidi ya lakini tatu, shule nane na vituo kadhaa vya kutolea huduma za afya mkoani Mara.


(Na Mobini Sarya, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages