SHIRIKA la Kimataifa la Vi-Agroforestry kwa kushirikiana na wadau, limeandaa Maneosho ya Sita ya Kilimo Mseto 2021, yatakayofanyika siku nne mfululizo katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Mseto (ATC) kilichopo Bweri, Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
“Maandalizi ya maonesho hayo yanaenda vizuri,” Afisa Miradi wa IDS, Davis Dominick amesema, juzi.
Dominick amesema mgeni rasmi katika maonesho hayo yenye kaulimbiu inayosema “Kilimo Mseto kwa Uhifadhi wa Mazingira na kipato”, anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo.
Mwenyeji wa maonesho hayo ni Kanisa AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kupitia shirika lake la Maendeleo la Inland Development Services (IDS).
Washiriki wa maonesho hayo ni mashirika yanayofadhiliwa na Vi Agroforestry, yakiwemo AICT MARA/IDS – Musoma, SHIMAKIUMU – Musoma, MAVUNO Karagwe – Kagera, ANSAF- Dar es Salaam, Inades Formation Tanzania - Dodoma na SCAAP - Mbeya.
Mengine ni BUFADESO – Bunda, FFS - Ukerewe – Mwanza, BRAC Tanzania, TACRI, Cafe Afrika, halmashauri za mkoa wa Mara, taasisi za fedha na mashirika ya umma.
Lengo kuu la maonesho hayo ni kueneza ujumbe kuhusu mchango wa kilimo mseto katika kuboresha hali ya maisha ya watu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Malengo mahususi ni kuwaleta pamoja washiriki wa sekta za umma na binafsi, zikiwepo taasisi mbalimbali zikiwemo zisizo za kiserikali zinazojishughulisha na mapambano ya kupunguza mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira kwa ujumla.
Pia, kushirikishwa tafiti mbalimbali zinazohusu mchango wa kilimo mseto katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na uboreshaji wa hali ya maisha kwa ujumla.
Lakini pia, kushiriki katika uchechemuzi wa kudai mkakati wa taifa wa kilimo mseto. “Mchakato huu umeanza kushughulikiwa na ofisi ya maliasili na utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na wameanza kuwashirikisha wadau kuandaa mkakati huo,” amesema.
Chimbuko la Shirika la VI-Agroforestry ni Sweden na katika Afrika Mashariki linafanya shughuli zake katika nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda.
(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)
No comments:
Post a Comment