BOMBA la maji yanayohofiwa kuwa na sumu - la mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, limepasukwa na kuzua taharuki kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime.
Tukio hilo limetokea katika barabara inayotumiwa na mgodi huo leo Aprili 23, 2022 saa nne asubuhi, kabla ya kudhibitiwa saa nane mchana.
Mara Online News imefika eneo la tukio na kushuhudia maji hayo yakitoka kwa kasi na kutiririka kuanzia maeneo ya makazi ya watu hadi kwenye kijito cha Nyamikoma kinachomwaga maji mto Tighite.
Mto Tighite unatiririkia kwenye Mto Mara ambao unamwaga maji katika Ziwa Victoria.
Baada ya kupata taarifa hizo, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amefika eneo la tukio akiwa amefuatana na wenyeviti wa vijiji na madiwani wa kata za Kewanja na Matongo kilipo kijiji cha Nyangoto.
Mbunge Waitara amempigia simu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko kumjulisha tukio hilo na baada ya dakika chache amefika eneo la tukio akiwa amefuatana na wasaidizi wake.
Alipoulizwa, Lyambiko ametangaza mbele ya Mbunge Waitara na umati wa wananchi waliokusanyika eneo la tukio hilo kwamba maji hayo ni machafu - yasiyostahili kwa matumizi ya binadamu.
Mbunge Waitara na wananchi wengine wakifuatilia mtiririko wa maji hayo
Baadaye Meneja huyo, Mbunge Waitara na wananchi wa kawaida wameongozana kufuatilia mtiririko wa maji hayo na kujiridhisha kuwa yameishia kwenye kijito cha Nyamikoma.
Mbunge Waitara amewaomba wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari ya kutotumia maji ya eneo la mto lililoingiliwa na maji hayo wakati wakisubiri majibu ya vipimo vya kitaalamu kujua kiwango cha sumu kilichomo.
“Maji haya yana tatizo, sasa ni sumu kiasi gani, hatujajua lakini maji yana sumu,” amesema Mbunge Waitara.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
Ni noma hiyo
ReplyDelete