NEWS

Monday 20 June 2022

Mashindano ya Kombe la Professor Mwera Foundation: Washindi wazawadiwa mabeberu ya mbuzi



MBUZI watatu ni miongoni mwa zawadi zilizotolewa kwa washindi wa mashindano ya Kombe la kumpongeza Mwasisi wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation (PMF), Peter Mwera.



Fainali za mashindano hayo zimechezwa Ijumaa iliyopita katika viwanja vya PMF mjini Tarime, ambapo baadhi ya timu za wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi na Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime zinazomilikiwa na taasisi hiyo, zimeng’ara.





Timu ya mpira wa miguu kwa wavulana wanaosoma Ufundi Magari (MVM) imejinyakulia zawadi ya beberu la mbuzi, baada ya kuibuka mshindi kwa kuinyuka timu ya Mafundi Umeme “Wakata Umeme” bao 1-0.


Kwa upande wa wasichana, timu ya soka ya Laboratory Assistant nayo imezawadiwa beberu la mbuzi, baada ya kuishinda timu ya Hotel and Tourism, zote za Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (Tarime Vocational Training College).


Fani zinazotolewa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime ni pamoja na ufundi umeme, magari, udereva, ushonaji na kompyuta.

Pia, wajumbe wa kamati ya maandalizi, uratibu na usimamizi wa mashindano hayo wameondoka na zawadi ya beberu la mbuzi.


Washindi wa pili wa mashindano ya mpira wa miguu na pete kwa timu za Chuo hicho na Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime (Tarime Girls Secondary School) wamepewa zawadi za soda.


Zawadi zote zimetolewa na Hezbon Peter Mwera ambaye ni Mkurugenzi wa Tasisi ya Professor Mwera Foundation, inayomiliki Tarime Girls Secondary School na Tarime Vocational Training College.

Aidha, mwanafunzi wa fani ya Uongozi wa Hoteli na Utalii (Hotel and Tourism), Mariam Masatu ameibuka mshindi wa jumla, baada ya kushinda katika michezo mingi, ikiwemo riadha, kula mkate na kunywa soda.



Mariam Masatu akipongezwa na Mkuu wa Chuo, Frank Joash aliyemwakilisha mgeni rasmi.

Mgeni rasmi wa mashindno hayo, Mwasisi wa Taasisi ya PMF, Peter Mwera, amewakilishwa na Mkuu wa Tarime Vocational Training College, Frank Joash.

Mwasisi wa Taasisi ya PMF, Peter Mwera

Joash amesema mashindano hayo yalianza mwezi uliopita, kwa lengo la kuenzi mchango wa Peter Mwera katika taasisi hiyo, lakini pia kuelekea Siku ya Baba Duniani (World Father’s Day) ambayo huadhimishwa Juni 19 kila mwaka.

Mwasisi huyo wa taasisi ya PMF pia Mkurugenzi wa Take Fish Farm, Radio Sachita FM na kituo cha afya Sachita mjini Tarime.



“Mashindano kama haya ni muhimu katika taasisi yetu kwani pia yanasaidia kutambua vipaji ya michezo miongoni mwa wanafunzi na wanachuo katika Taasisi yetu ya Professor Mwera Foundation,” amesema.

Joash ametumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha watu kwenda klabu ya mazoezi ya viungo katika taasisi PMF inayojulikana kwa jina la Serengeti Jogging Club.



Mwaka jana, taasisi ya Professor Mwera Foundation ilizipatia shule bora mkoani Mara tuzo zenye thamani ya shilingi milioni 12, kwa kukishirikiana na ofisi za Afisa Elimu na Mkuu wa Mkoa.

Pia, hivi karibuni taasisi hiyo imetoa tuzo kwa shule bora katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Simiyu na Geita.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila (kulia), akimtunuku Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera cheti cha pongezi na kutambua mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya elimu mkoani hapo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, anasema taasisi hiyo imeidhinishwa na Serikali kuendesha programu ya mafunzo ya kitaaluma kwa wafanyakazi wa sekta za hoteli na utalii katika mikoa 10.

“Mikoa hiyo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvuma,” amesema Hezbon ambaye pia ni mmoja wa wanachama wa chama tawala - CCM waliotia nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.

“Vijana waliopata daraja la nne na alama sifuri wana fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili wasijione wametengwa… kupitia vyuo vya ufundi wanaweza kupanda hadi chuo kikuu na hatimaye kuajiriwa, au kujiajiri kutokana na fani walizosoma,” anasema.

Mkurugenzi Hezbon anaongeza “Tunahamasisha vijana baada ya kumaliza kidato cha nne wakati wanasubiri matokeo ni vizuri wakajiunga na vyuo vya ufundi wakapata zile fani, matokeo yakitoka yakiwa mazuri, kijana akienda Advance (kidato cha tano) akiwa na fani yake kuna sehemu itamsaidia.

“Lakini matokeo yasipokuwa mazuri, ile fani pia anaweza akajiendeleza nayo na baadaye ikamsaidia kujiajiri au kuajiriwa. Kwa hiyo tuhamasishe vijana kuona umuhimu wa kujiunga na hivi vyuo vya ufundi ambavyo kwa sasa vimeunganishwa na NACTE ili kuviboresha kitaaluma.”

Hezbon anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuiletea nchi maendeleo ya kisekta, ikiwemo kutoa fursa kwa watoto wa kike kuendelea na masomo baada ya kuwa wamekatishwa kwa kupata ujauzito na kujifungua.

Anasema Tarime Vocational Training College ni moja ya vyuo vikubwa Kanda ya Ziwa, na tayari kimeanzisha mpango wa kusaidia vijana kusoma bure na kwamba hadi sasa kimeshasaidia vijana zaidi ya 3,000.



“Ninamshukuru na kumpongeza Mama [Rais Samia] kwa kufungua mipaka na kuleta fursa nyingi kwa Tanzania na kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake, Dkt John Pombe Magufuli.

“Nampongeza Rais wetu pia kwa maono makubwa ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Tunaona juhudi zake katika shule - ametoa fedha za kujenza madarasa ili kuongeza fursa kwa watoto wengi kupata elimu,” amesema Hezbon.

Anaongeza kuwa Rais Samia pia anastahili pongezi kwa kuonesha dhamira ya kuanzisha vyuo vya ufundi kila wilaya nchini.

“Vyuo hivi vitasaidia vijana wengi waliohitimu kidato cha nne, kukata tamaa na kuzurura mitaani kutokana na kukosa ajira,” anasema Hezbon.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages