Na Mwandishi Wetu, Musoma
----------------------------------------
MAANDALIZI ya Meonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Mkoa wa Mara yanayojulikana kwa jina la Mara International Business Expo 2022 yamekamilkka kwa asilimia 99.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema leo mjini Musoma kuwa taasisi na kampuni kubwa zaidi ya 100 zimethibitisha kushiriki maonesho hayo.
Ndengo amefafanua kuwa maonesho hayo yataanza Septemba 2, mwaka huu na yanatarajiwa kuzinduliwa na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
“Tayari tumepewa kibali na Seriali kwa ajili ya kuendesha maonesho haya na ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetueleza kuwa Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ndiye atamwakilisha Rais wa Tanzania katika ufunguzi wa maonesho yetu,” amesema.
Ametaja baadhi ya kampuni na taasisi zilizothibitisha kushiriki maonesho hayo yanayolenga kutangaza utalii na fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani Mara kuwa ni pamoja na Barrick, Grumet Reserves na benki zikiwemo CRDB, NBC na TCB.
Ndengo ametaja taasisi nyingine zilizothibitisha kushiriki maonesho hayo kuwa ni pamoja Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), TEMESA na Costech, huku wajasiriamali wadogo na wa kati 300 wakitarajiwa kushiriki.
Mwenyekiti huyo wa TCCIA Mara amesema pia balozi za Zimbabwe na Malawi zimethibitisha kushiriki huku wakitarajia wageni mbalimbali kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza na kutoa uzoefu wao kwa washiriki.
Amesema maonesho hayo ambayo kwa sasa yanatarajiwa kushirikisha washiriki wa ndani na nje ya nchi yatakapomalizika yatakuwa yameutangaza mkoa wa Mara na fursa zilizopo kwa ajili ya uwekezaji na biashara.
“Hili tunalolifanya ni moja ya jukumu letu sekta binafsi, tuna wajibu wa kuisaidia Serikali katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na uchumi imara, sasa tunakwenda kutumia mitandao yetu kwenye nchi zote duniani kufanikisha maonesho haya ambayo yanatarajiwa kushirikisha watu kutoka mataifa mbalimbali duniani,” amesema Ndengo.
No comments:
Post a Comment