
Muonekano wa sehemu ya mbele ya The Silver Spring Hotel - Nyamongo
----------------------------------
Kwa sasa, ukizungumzia suala la hoteli ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa katika eneo maarufu la Nyamongo ‘habari ya mjini’ ni The Silver Spring Hotel.
The Silver Spring Hotel, ni hoteli mpya ya kisasa iliyojengwa na mwekezaji mzawa katika ardhi iliyojaaliwa utajiri mkubwa wa dhahabu katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Hotel hii ilifungua milango kwa wageni Februari 14, 2026 na hivyo kupaisha hadhi ya eneo maarufu la Nyamongo linalovutia wawekezaji katika sekta ya madini kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na kuwa katika eneo lenye hekaheka za biashara ya dhahabu, hoteli hii pia ipo jirani na njia muhimu ambayo watalii wa kigeni kutoka mataifa mbalibali wanapita kuelekea hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Aidha, ukisimama juu ya ghorofa ya The Silver Spring Hotel - Nyamongo unaweza kutazama kwa mbali hifadhi hiyo maarufu duniani.

Hakika, ubunifu wa jengo lake la kisasa lenye ghorofa kadhaa na mandhari ya kuvutia, The Silver Spring Hotel inaakisi upekee wake unaovutia macho ya kila mgeni.
“Ni hoteli yenye hadhi ya nyota tano ambayo tumewajengea wageni - wanapokuja wapate sehemu sahihi ya kupumzika,” Mkurugenzi wa The Silver Spring Hotel, Godfrey Emmanuel Kubyo, alisema katika mazungumza na waandishi wa habari waliotembelea uwekezaji huo wiki iliyopita.
Wanahabari hao zaidi ya 30 waliongozwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), jacob Mugini.

Msimamizi wa vyumba vya kulala wageni wa hoteli hiyo, Neema John Ngaila, anasema vyumba hivyo vimejengwa kwa ustadi na usalama wa hali ya juu - vikiwa na samani za kifahari na huduma nyingine muhimu zinazokidhi mahitaji ya mteja.
Neema anasema mbali na kuwa na vitanda, meza na viti vya kisasa, vyumba hivyo vina runinga za kisasa na huduma ya Wi-Fi ya uhakika inayomwezesha mgeni kuendelea na shughuli zake za kikazi bila kikwazo.
Anataja huduma nyingine kuwa ni pamoja na restaurant ya kisasa ambapo wateja wanapata vyakula vya asili na vya kimataifa vilivyoandaliwa na wapishi waliobobea, pamoja na baa ya kisasa yenye vinywaji vya aina zote katika mazingira tulivu na yenye mvuto.

The Silver Spring Hotel si mahali pa kulala, kula na kunywa pekee, bali pia kuna huduma za sauna na saluni/ barbers hop za kisasa zenye wahudumu wabobezi, eneo kubwa la maegesho ya magari, gym yenye vifaa vya kisasa na kumbi za mikutano zenye teknolojia ya kisasa.
Pia, huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi katika hoteli hii ambayo kwa mujibu wa Mkurugenzi wake, Kubyo, imeimarishiwa usalama mkubwa wakati wote.

Meneja Masoko na Mauzo, Jesca Paul, anasema “Ukija The Silver Spring Hotel utapata huduma zote ambazo hutalazimika kwenda kuzipata nje.”
Jesca anawahakikishia wageni kuwa hawatajuta kwenda kupata huduma za hoteli hiyo kwani ni mahali panapofaa kwa mapumziko ya familia, hafla maalum, au hata picha za kumbukumbu zenye mvuto wa asili.
“Mazingira yetu ni makubwa ya kutosha, unaweza ukakaa sehemu yenye hekaheka na sehemu ambayo ni tulivu, tuna gadeni, kwa wale wanaohitaji sehemu iliyotulia unaweza ukakaa sehemu iliyojificha ukafanya mambo yako kwa utulivu,” anaongeza.

Mkurugenzi wa The Silver Spring Hotel, Kubyo na Meneja wa hoteli hii, Dankani Kakai, wanawakaribisha wageni wote kupanga kwenda kufurahia huduma bora za aina yake.
“Hii ni hoteli yenye hadhi ya nyota tano, tunaomba muwe mabalozi wetu wazuri popote pale mtakapokuwa,” Mkurugenzi Kubyo anawambia waandishi wa habari.
Wakazi wa mji wa Nyamongo hivi sasa wanajivunia uwepo wa hoteli hii katika maeneo yao.
“Kwa kweli Godfrey Kubyo ameweka alama, kwa sasa mtu akifika Nyamongo bila kufika The Silver Spring Hotel anakuwa hajafika Nyamongo,” anasema Marwa Mwita, mwendesha bodaboda katika mji huo.

Kwa kifupi, The Silver Spring Hotel ni fahari ya Nyamongo, ni mahali sahihi kwa yeyote anayehitaji huduma bora za malazi, chakula, vinywaji, mikutano, burudani na mapumziko ya kifahari katika eneo la kimkakati lenye umuhimu mkubwa kiuchumi.
Hivyo basi, ukitaja hoteli bora ya kisasa na yenye hadhi ya kimataifa katika mji maarufu wa Nyamongo, jibu ni moja tu: The Silver Spring Hotel, fahari ya Nyamongo.

No comments:
Post a Comment