NEWS

Thursday, 11 August 2022

Polisi Tarime-Rorya wakamata magunia 67 ya bangi na watuhumiwa 110 wa uhalifu mbalimbali




Na Mara Online News
----------------------------

JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya limefanikiwa kukamata magunia 67 ya bangi yenye uzito wa kilo 3,350 na mawe mawili yanayodhaniwa kuwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 200.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Geofrey Sarakikya (pichani juu katikati), amewambia waandishi wa habari ofisini kwake leo Agosti 11, 2022 kwamba wanashikilia pia watuhumiwa na magari yaliyokuwa yamebeba bidhaa hizo.


Kamanda Sarakikya akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) magunia 67 ya bangi waliyokamata

ACP Sarakikya amefafanua kuwa bangi hiyo ilikamatwa juzi saa 11:40 jioni katika kijiji cha Nyamwigura, ikiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 597 CFY aina ya Fusso, mali ya Festo Mmassy, mkazi wa Arusha.

“Mbinu iliyotumika ni kuyaficha magunia hayo ndani ya gari kwa kuyafunika kwa mikungu ya ndizi mbichi… uchunguzi wa awali umebaini kuwa bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam,” amesema Kamanda Sarakikya.


Kamanda Sarakikya akiwaonesha waandishi wa habari mikungu hiyo

Ameongeza kuwa gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Samson Mollel ambaye hata hivyo alitoroka na kuwaacha wenzake wawili wanaoshikiliwa na polisi.


Kamanda Sarakikya akiwaonesha waandishi wa habari gari hilo

Amesema mawe mawili yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, nayo yalikamatwa na polisi siku hiyo hiyo saa 12 jioni katika kitongoji cha Forodhani kilichopo Sirari mpakani na nchi ya Kenya, yakiwa yamefichwa ndani ya gari lenye namba za usajili KDH 718 T aina ya Land Cruiser Prado.

Kwa mujibu wa ACP Sarakikya, mmiliki wa gari hilo ni raia wa Kenya aliyejulikana kwa jina moja la Matiko na kwamba mawe hayo yalikuwa yanatoroshwa kwenda nchi jirani.

Amesema watuhumiwa wawili kuhusiana na tukio hilo walikamatwa na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha, Kamanda huyo amesema jeshi hilo pia limefanikiwa kubaini na kukamata mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 74.2, mirungi yenye uzito wa kilo 292 na watuhumiwa 110 wa uhalifu kati ya Januari na Julai mwaka huu katika Wilaya za Kipolisi za Tarime, Sirari, Nyamwaga, Kinesi, Shirati na Rorya.

“Kesi za watuhumiwa hao ziko katika hatua mbalimbali za kisheria,” amesema ACP Sarakikya na kuweka wazi kuwa hali ya Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya ni shwari.


Picha zote na Mara Online News

Kamanda Sarakikya amesema polisi wanaendelea na juhudi za kuwatafuta ili kuwatia mbaroni watuhumiwa wengine kuhusiana na matukio hayo waliotoroka.

Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya kulima, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya, la sivyo wataishia mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.

“Tutawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahalifu wote ambao taarifa zao zitatufikia,” amesisitiza Kamanda Sarakikya na kuwashauri wananchi kufanya kazi halali ili kujipatia kipato.

Pia ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kama vile magari na pikipiki kuhakikisha havitumiki kusafirisha dawa za kulevya na bidhaa nyingine za kihalifu, kwani vikikamatwa vitataifishwa kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Sarakikya amehitimisha kwa kuwaomba wananchi wema kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kukomesha uhalifu, hivyo kuwezesha umma kuendelea na shughuli za kiuchumi na kuishi kwa usalama na amani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages