NEWS

Monday 23 January 2023

Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Halmashauri ya Rorya yabaini dosari kwenye mradi wa lambo uliotumia fedha za Mfuko wa Jimbo


Na Mwandishi Wetu, Rorya
-------------------------------------------

KAMATI ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imebaini dosari katika utekelezaji wa mradi wa lambo la maji ya mifugo uliodaiwa kutekelezwa katika kijiji cha Radienya kwa gharama ya shilingi milioni tatu zilizotolewa na Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.

“Fedha zimefika Radienya kuchimba lambo - zikatengeneza kinga maji, ni nani aliyebadilisha matumizi kutoka lambo kwenda kinga maji?

“Tumewashirikisha wataalamu watuongoze, kila mmoja anashangaa kilichofanyika, mshangao huu unatutia mashaka makubwa. Fedha ilitoka kwa ajili ya mradi wa lambo lakini hili siyo lambo.

“Tunapoambiwa kuna kata tano ina maana kuna milioni 15 zimepitishwa kuchimba malambo kwenye kata tano wakati Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala haina taarifa hiyo,” Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Gerald Ng’ong’a alisema baada ya kuongoza Kamati hiyo kukagua mradi huo kijijini Radienya, hivi karibuni.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Ng’ong’a aliouagiza uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Radienya kuwasilisha kwa Kamati ya Fedha maelezo ya kimaandishi ya sababu za kubadilisha ujenzi wa lambo kuwa wa kinga maji.

“Mtendaji wa kijiji, mwenyekiti wa kijiji, serikali ya kijiji mtuambie aliyewaruhusu kubadilisha matumizi, badala ya lambo mkajenga kinga maji, leteni hayo maandishi.

“Sisi kama Kamati, kwa taarifa za fedha zilizotolewa kwa ajili ya lambo - hili siyo lambo. Kwa hiyo ina maana fedha zilizoletwa kwa ajili ya lambo bado zipo,” Ng’ong’a alisisitiza.
Mwenyekiti Gerald Ng'ong'a

Zaidi ya hayo, wataalamu wa serikali kutoka sekta husika walisema hawakushirikishwa katika mipango na maandalizi ya ujenzi wa lambo kwa ajili ya maji ya mifugo katika kijiji cha Radienya.

Afisa Mifugo wa Halmashauri hiyo, Mashigole Jumbe alisema hakushirikishwa katika maandalizi ya mradi huo na kusisitiza kuwa shilingi milioni tatu hazitoshi kugharimia uchimbaji wa lambo.

“Huu mfuko wa Jimbo kwangu ni changamoto, ni changamoto kwa sababu fedha zilipopangwa mimi sikushirikishwa. Kwamba milioni tatu zinajenga lambo mimi sijawahi kushirikishwa,” Afisa Mifugo wa Halmashauri hiyo, Mashigole Jumbe alisema.

“Baadaye nilipokuja kushirikishwa nikamwambia injinia twende kuona malambo ambayo yatajengwa kwa milioni tatu, lakini baadaye tukagundua kwamba hizo milioni tatu hazitoshi kujenga lambo.

“Tukawambia sisi hatutashiriki kwenye ujenzi kwa sababu injinia ameshindwa kutengeneza BOQ ambayo inaweza kutosha shilingi milioni tatu. Kwa hiyo, kifupi kwa kweli sijawahi kushiriki kupanga kwamba milioni tatu inatosha lambo.

“Sijawahi kushiriki kupanga, milioni tatu hazitoshi lambo, hili tuta hata maji yakitoka huko mengi yanakata tu hata hamna cha kuzuia,” alisema mtaalamu huyo aliyewekwa na serikali kusimamia maendeleo ya sekta ya mifugo katika halmashauri hiyo.

Nao baadhi wa wajumbe wa Kamati hiyo ambao ni madiwani, walilaani kitendo cha Kamati ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Rorya kupanga utekelezaji wa miradi ya umma bila kushirikisha wataalamu, wakisema ni upotevu wa fedha za serikali.

“Hili ni kinga maji siyo lambo, lambo lina utaratibu wake wa ujenzi, hata kinga maji lina namna yake - lazima lishindiliwe ili liyakinge kweli maji, sasa hii haikingi maji, yatakapokuja yatapita tu kwa sababu ni mchanga tu umesimamishwa hapo haujashindiliwa, haujashikana. Kwa hiyo maji yakijaa yatatoka tu na hatutaki serikali ionekane inababaisha,” Albert Nguchiro.
Muonekano wa kinga maji lililojengwa katika kijiji cha Radienya. (Na Mpigapicha Wetu)

Mjumbe mwingine alisema “Kama Afisa Mifugo mwenye kitengo anakiri kuwa fedha hii milioni tatu ni ndogo, ninachokiona ni kuwa Kamati ya Mfuko wa Jimbo ilitenga fedha bila kujua thamani halisi ya mradi. Kama kitu hakiwezekani ni bora kisubiri kuliko kutengewa fedha ambayo haitoshi, maana kinachoenda kutekelezwa kinakuwa chini ya kiwango na kuleta sintofahamu.”

Awali, Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Radienya, Rhoda Nyabukika alisema utekelezaji wa mradi huo umesuasua kwa muda mrefu baada ya mtu waliyemtegemea kusaidia kuchimba lambo hilo kukataa.

“Tulidhani mradi huu ungetekelezwa kwa urahisi kwa kutumia mkandarasi aliyekuwa anajenga madaraja ya mto Mori. Tuliwasiliana nao wakaonesha wangetupa msaada lakini hawakuweza kutusaidia shughuli hii,” alisema Rhoda kwenye sehemu ya taarifa yake kwa Kamati ya Fedha.

VEO Rhoda alisema baada ya kukaa na fedha muda mrefu waliamua kukodi mashine kwa shilingi milioni 2.5 na shilingi 460,000 zilitumik kununua mafuta kwa ajili ya kujenga kinga maji.

Kwa mujibu wa taarifa ya VEO Rodha, mradi huo ni miongoni mwa miradi mitano ambayo ilitengewa shilingi milioni 15 na Kamati ya Mfuko wa Kuchochea Mendeleo ya Jimbo katika kata tano ikiwemo ya Kirogwe kilipo kijiji cha Radienya.

Akirudia kauli yake, Mwenyekiti Ng’ong’a alisisitiza kuwa fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya uchimbaji wa malambo matano jimboni humo bila kufuata utaratibu wa kuishirikisha Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango.

Alipoulizwa na Sauti ya Mara kwa njia ya simu wiki iliyopita, Mbunge wa Rorya, Jafari Chege alidai kuwa Kamati ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo haiwajibiki kuishirikisha Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango - wala Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya katika maandalizi ya miradi ya maendeleo ya wananchi.

Hata hivyo Chege alikiri kuwa shilingi milioni tatu haziwezi kutosha kugharimia uchimbaji wa lambo la maji na kuongeza kuwa wananchi wa maeneo husika walipaswa kuchangishana ili kupata kiasi kinachotosha kugharimia ujenzi huo.

Mbunge Jafari Chege

“Mfuko wa Jimbo unasaidia tu nguvu za wananchi… wao wanatakiwa waongezee ili kuchimba lambo. Kwa hiyo kama ilikwenda milioni tatu walitakiwa sasa waongezee kulingana na bajeti yao,” alisema Chege.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages