Na Mwandishi Wetu
-----------------------------
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimezindua maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho, huku wabunge 11 wanaotokana nacho mkoani humo wakishindwa kuhudhuria.
Uzinduzi huo ulifanyika kimkoa katika uwanja wa “Shamba la Bibi” wilayani Tarime jana, mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi.
Kati ya wabunge 13 wa mkoani Mara wanaotokana na CCM, wakiwemo 10 wa majimbo na watatu wa viti maalum, ni wawili pekee waliohudhuria uzinduzi huo.
Uchunguzi uliofanywa na Mara Online News wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM, ulibaini kuwa wabunge pekee waliohudhuria ni Mwita Waitara wa Jimbo la Tarime Vijijini na Michael Kembaki (Jimbo la Tarime Mjini).
Mbali na wabunge watatu wa viti maalum, majimbo manane ya mkoani Mara ambayo wabunge wake wa CCM hawakutia unyayo katika uzinduzi huo kwa sababu ambazo hazikujulikana haraka, ni Serengeti, Rorya, Butiama, Musoma Mjini, Musoma Vijijini, Bunda Mjini, Bunda Vijijini na Mwibara.
Waitara na Kembaki walitumia fursa hiyo ya uzinduzi huo kuwaeleza wananchi miradi mbalimbali ya kisekta iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa katika majimbo yao chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya CCM mkoani Mara vinasema hiyo si mara ya kwanza kwa baadhi ya wabunge wa mkoani Mara kushindwa kuhudhuria mikutano na vikao vinavyojadili masuala muhimu ya maendeleo ya chama hicho tawala.
“Mfano baadhi wabunge wengi hawakuhudhuria kikao cha kwanza cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara baada ya uchaguzi wa viongozi wa CCM kumalizika, kilichofanyika Desemba 15, mwaka jana,” amesema mmoja wa makada wa chama hicho mkoani Mara.
Miezi michache iliyopita, baadhi ya wananchi wakiwemo wanachama wa CCM walikosoa vikali tabia ya baadhi ya wabunge wa mkoani Mara kugeuza makatibu wao kuwafanyia kazi za kibunge.
Watu wengi walijitokeza kukosoa tabia hiyo baada ya makatibu waliokuwa wamewawakilisha wabunge wao kutimuliwa kwenye kikao kilichokuwa kinajadili maendeleo ya mkoa wa Mara, ambacho kisheria makatibu wa wabunge siyo wajumbe halali wa kikao hicho.
Waliwanyooshea kidole wabunge wanaoendekeza tabia hiyo wakisema kitendo cha kuwageuza makatibu wao kuwa wabunge wa wananchi ni dharau na hakina afya kwa maendeleo ya mkoa wa Mara.
Vyanzo vyetu vinadai kuwa baadhi ya makatibu wa wabunge hao wamejigeuza kuwa wajumbe wa vikao vya kisheria vya ngazi ya mkoa na mabaraza ya halmashauri za wilaya, miji na manispaa, huku wakilipwa posho kama ilivyo kwa wabunge.
No comments:
Post a Comment