Na Mara Online News
----------------------------------
MGODI wa Dhahabu wa North Mara umeshirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tarime kuwapatia madereva wa pikipiki za abiria (bodaboda) elimu ya usalama barabarani, ili kuepusha ajali katika maeneo yaliyo jirani na mgodi huo.
Hayo yamejiri leo Machi 17, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, yaliyofanyika kiwilaya katika mji mdogo wa Nyamongo uliopo jirani na mgodi wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mgodi huo umetumia nafasi hiyo pia kugawa msaada wa kofia ngumu 100 na jaketi maalumu 200 kwa baadhi ya waendesha bodaboda, huku Jeshi la Polisi likitumia vifaa mbalimbali kuwaelimisha sheria na alama za usalama barabarani.
Mkuu wa Kitengo cha Polisi wa Usalama Barabarani Wilaya ya Tarime, ASP Barnabas Irumba amesema ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na madereva wa bodaboda wasio na elimu ya matumizi ya vyombo vya moto barabarani.
“Waathirika wakubwa wamekuwa ni waendesha bodaboda wasio na elimu ya kutosha na abiria wanaowabeba. Ajali hizi zimekuwa zikichangia ongezeko la wajane na watoto yatima katika jamii yetu,” amesema ASP Irumba.
Hata hivyo amesema jeshi hilo lina mkakati ya kuboresha usimamizi wa usalama barabarani, ikiwa ni pamoja kuelimisha madereva wa bodaboda na watembea kwa miguu wakiwemo wanafunzi, kukagua vyombo vya moto na kupiga marufuku visivyofaa kutumika barabarani.
Awali, viongozi wa vijiji na kata jirani walikemea matumizi holela ya vyombo hivyo vya moto na kuwataka vijana waliojiajiri katika sekta hiyo kubadilika kwa kuhakikisha wanapata mafunzo stahiki na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
“Fuateni sheria za barabarani na kuchukua tahadhari zote, ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo vya moto mkiwa mmetumia pombe na dawa za kulevya. Pia acheni kuvaa ndala, vaeni viatu vigumu na helmenti (kofia ngumu), amesisitiza Diwani wa Kata ya Kibasuka, Thomas Nyagoryo.
Mwakilishi wa maofisa watendji wa vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, James Magige amewakumbusha waendesha bodaboda kuzingatia pia suala la kuwa na leseni ya udereba na kuepuka mwendo kasi barabarani.
Kwa upande wao, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Paul Bageni (Mjini-Kati) na Mwalimu Mwita Msegi (Nyangoto) wameuomba kujenga matuta maalumu na kuweka alama za vivuko vya waenda kwa miguu kwenye barabara ya lami ili kupunguza ajali katika mji wa Nyamongo.
Naye mwakilishi wa waendesha bodaboda waliohudhuria kilele hicho cha maashimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, aliyejitambulisha kwa jina la Msofe, ameushukuru mgodi wa North Mara kwa msaada wa kofia ngumu na jaketi maalumu, na kwa upande mwingine Jeshi la Polisi kwa mafunzo ya sheria za barabarani, huku akiomba utaratibu uwe endelevu ili kujenga mahusiano baina yao.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment