NEWS

Sunday 5 March 2023

Kamati ya Siasa CCM kuhitimisha ziara ya ukaguzi wa miradi Tarime Mji leo



Na Mara Online News
--------------------------------

KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, leo inatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya siku mbili ya kukagua miradi ya kijamii inayotekelezwa na Serikali katika Halmashauri ya Mji wa Tarime inayoongozwa na Mkurugenzi Gimbana Ntavyo.

Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake, Marwa Daudi Ngicho, ambapo katika ziara ya jana ilikagua Shule ya Sekondari mpya ya Mogabiri, Kituo cha Afya Kibumaye, mradi wa maji Gimenya na daraja la Mori, miongoni mwa miradi mingine.
Mwenyekiti Ngicho (wa pili kushoto) na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime wakifuatilia jambo wakati wa ziara ya kukagua miradi katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Kwa ujumla Kamati hiyo ilieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa maelekezo mbalimbali ya kuweka msukumo wa kuikamilisha kwa wakati ili iweze kuhudumia wananchi.

“Nimefurahi kuona ujenzi wa daraja la Mori, ni kubwa na la kisasa, likikamilika litawaondolea wananchi tatizo la kusombwa na maji, lakini pia litawarahisishia usafiri,” alisema Mgicho.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (wa pili kushoto mwenye kofia), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo (wa pili kulia) na Katibu wa CCM Wilaya, Valentine Maganga (kulia) wakifurahia jambo walipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Mori.

Daraja hilo ambalo linaungnisha kata ya Nkende na Kitare, ujenzi wake umetengewa shilingi zaidi ya milioni 600 kutoka serikalini, na unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tarime.

Ngicho alitumia nafasi hiyo pia kuelekeza viongozi husika kuingiza daraja hilo kwenye orodha ya miradi ya maendeleo ya wananchi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta shilingi milioni 675 kujenga daraja hili la Mori kwa manufaa ya wananchi wetu. Kwa ujumla utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Mji wa Tarime unaenda vizuri.

“Tumekagua na kujiridhisha kuwa pesa zinazoletwa na Serikali kwenye wilaya yetu ya Tarime zinafanya kazi zilizokusudiwa - kuanzia kwenye madarasa ya shule, barabara hadi kwenye miradi ya maji na afya, kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi za miradi Tarime," Ngicho alisisitiza.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime, aliwataka wataalamu kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo, kwa kusimamia na kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi kupata huduma stahiki.

Juzi, Kamati hiyo ilihitimisha ziara yake ya siku tatu ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) inayoongozwa na Mkurugenzi Solomon Shati.

Ukaguzi wa miradi ukiendelea

Mbali na Wakurugenzi Gimbana wa Tarime Mji na Shati wa Tarime Vijijini, katika ziara hizo Mwenyekiti Ngicho alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Wabunge Michael Kembaki wa Tarime Mjini na Mwita Waitara (Tarime Vijijini), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles, miongoni mwa wajumbe wengine wa kamati hiyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages