Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inavyoonekana unapokuwa juu ya milima ya Nyanungu
Na Mwandishi Maalumu
--------------------------------------
WAKAZI wa vijiji vya Kegonga na Nyandage vilivyopo kata ya Nyanungu wilayani Tarime, Mara, wamesema wako tayari kukaribisha wawekezaji wa hoteli na kambi za kitalii katika eneo lao linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hata hivyo wamesema kinachochelewesha hatua hiyo ni uwekaji wa vigingi vya mpaka unaowatenganisha na hifadhi hiyo.
Wanaamini uwekezaji huo utakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi ya vijiji hivyo, hasa ikizingatiwa kuwa havijawahi kuwa na vyanzo vya mapato tangu vianzishwe, na hali ya maisha ya wengi wao ni duni huku wakikabiliwa pia na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kama vile maji, afya na elimu.
“Tunahitaji suluhu ya mvutano wa mpaka unaotenganisha vijiji vyetu na Hifadhi ya Serengeti, tunaomba Serikali iwahishe uwekaji wa vigingi vya mkapa huo, tujenge mahusiano mazuri na hifadhi na kukaribisha wawekezaji,” amesema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kegonga, Waryoba Mogoyo katika mahojiano na timu ya Sauti ya Mara iliyotembelea vijiji hivyo, hivi karibuni.
Mogoyo anaweka wazi kuwa matamanio ya wakazi wa vijiji hivyo ni kuona wanashirikishwa kikamilifu katika suala zima la utatuzi wa mgogoro uliopo, ili waanze kujielekeza kwenye mpango wa kukaribisha wawekezaji.
“Tushirikishwe, hata kwenye buffer zone (eneo kinga la hifadhi) tujue sisi wananchi tunafikia wapi. Ni muhimu tujue mpaka wetu ili hata watoto wetu anapokwenda kuchunga [mifugo] wawe wanajua mpaka wa maeneo yetu.
“Tukishaoneshwa mpaka wa eneo letu na kuwekewa bacons (vigingi) tutahitaji wawekezaji kwa sababu tutafunga nao mkataba na vijiji vyetu vitapata mapato na maendeleo, hivyo kuona faida ya uhifadhi na uwekezaji,” anasema kiongozi huyo.
Kwa upande mwingine wanavijiji hao wanasema wako tayari kuhuisha mahusiano na ujirani mwema na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa maendeleo yao na uhifadhi.
“Miaka ya nyuma tulikuwa na mahusiano mazuri, TANAPA walitujengea madarasa ya shule na kutuboreshea kisima. Kwa hiyo sisi tunawakaribisha waje mazungumzo yafanyike mbele ya wananchi kwenye eneo la mgogoro, suluhu ipatikane tujielekeze kwenye masuala ya maendeleo,” Mogoyo anasisitiza.
Mwenyekiti wa chama tawala - CCM Kata ya Nyanungu, Kimunye Chacha anasisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro wa kugombea mpaka kati ya wanavijiji na Hifadhi ya Serengeti unahitajika haraka kwani unachelewesha maendeleo ya vijiji vya Kegonga na Nyandage, ikiwemo kukaribisha wawekezaji.
“Serikali inatakiwa ifanye maamuzi haraka ili kila upande ujue mpaka wake. Tunahitaji mazungumzo na maridhiano, na mhimili utakaosimamia hayo ni Serikali, vinginevyo kuchelewesha maamuzi ya mpaka kunatoa mwanya kwa kila upande kujiona una haki ya kutumia eneo linalogombewa,” anasema Kimunye.
Kimunye pia anaunga mkono wazo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee la kuwataka wanavijiji kuangalia uwezekano wa kutenga maeneo yao yanayopakana na Hifadhi ya Serengeti, kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli na kambi za kitalii.
“Uwekezaji hakuna anayeukataa, mpaka ukishajulikana utatusaidia kutenga eneo la kukaribisha mwekezaji ili kila upande unufaike,” anasema Kimunye na kuendelea:
“Lakini kikubwa, wakitaka huu mgogoro uishe, ni kiasi cha kumshirikisha mbunge, diwani, viongozi wa kata, viongozi wa vijiji na wazee wa mila wakae sehemu wabainishe mambo yote umuhimu, hao watu watakaporudi kwa wananchi wanaweza wakawa kitu kimoja na Serikali pamoja na wananchi, amani ikapatikana mahusiano yakajengeka.”
“Mbunge akija akatwambia jamani ee kufuga (mifugo) na kuwa na wawekezaji wa hoteli za kitalii hapa kuna faida moja, mbili, tatu, na ukweli hata mimi [Kimunye] najua bila mbunge kunishauri wala mtu wa Serikali kunishauri, uwekezaji una faida kuliko mambo ya ufugaji.
“Lile eneo [linalogombewa] ni dogo kwenye mambo ya ufugaji, tukisema tuamue kufuga halitatosha, lakini kwenye uwekezaji linatosha na faida ni kubwa - tutapata fedha na vijana watapata ajira. Lakini shida ni kutoshirikisha uongozi, hiyo ndiyo shida moja tu, washirikishe viongozi wetu mawasiliano yawepo ambayo hayana kona, sisi tuko tayari,” Kimunye anasisitiza.
Kuhusu kama ikitokea Serikali ikaamua kuhamisha baadhi ya wanavijiji ili kupisha uhifadhi, Kimunye anasema “Mhimili wa Serikali ukiamua itabidi tukubaliane na hayo maamuzi.”
Naye mkazi wa kijiji cha Kegonga, Ester Massa anakiri kuwa uwekezaji utakuwa mkombozi wao wa kiuchumi kutokana na ajira mbalimbali zitakazopatikana kwenye hoteli na kambi za kitalii.
“Tukipata wawekezaji, vijana wetu wakiwemo mabinti watapata ajira, hata wazee wenye uwezo watapata ajira maana wanakijiji wengi hatuna sehemu ya kujipatia fedha. Kikubwa tuelimishwe faida za uwekezaji, sisi tuko tayari,” anasema Ester.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyandage, Mwita Kiya Rokomo anaunga mkono mtanzamo wa wakazi hao wa kijiji cha Kegonga, akisema wananchi katika kijiji chake poa wana shauku kubwa ya kuona mgogoro wa kugombea mpaka umalizika haraka ili waanze kufaidi matunda ya uwekezaji wa kitalii.
“Hali ya maendeleo ya kijiji chetu ni ya kiwango cha chini, kwa sababu ni maendeleo ya mtu mmoja mmoja, watu wengine maendeleo ni ya chini sana,” anasema Rokomo na kuongeza:
“Kijiji changu pia hakina chanzo cha mapato, tunakubali wazo la kukaribisha wawekezaji. Tunachoomba mgogoro uliopo utatuliwe ili mkanganyika wa kuingiliana na hifadhi uishe. Wana-Nyandage tuko tayari kupokea wawekezaji watusaidie kutatua changamoto zinazotukabili, lakini pia tujenge mahusiano yetu na majirani zetu wa Hifadhi ya Serengeti.”
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngori kilichopo kijiji cha Nyandage, Nyamsabi Marwa anasema mgogoro uliopo umechangia maisha duni ya wananchi katika kitongoji na kijiji hicho.
Hivyo Marwa anaomba mgogoro huo utatuliwe haraka iwezekanavyo ili wajipange kukaribisha wawekezaji kwa ajili ya kupata maendeleo ya kisekta.
“Hatupingi uwekezaji kwani kupinga uwekezaji ni kupinga maendeleo. Ili tupate maendeleo lazima ushirikiano na hifadhi uwepo pia tutatue kero zetu kwa pamoja, maana sasa hivi huduma za kijamii ni duni sana katika kijiji chetu.
“Kwa hiyo sisi tunahitaji kuunganishwa na hifadhi kimahusiano na ujirani mwema, kisha wawekezji waje kuwekeza kwenye maeneo yetu yanayopakana na hifadhi ili tupate maendeleo,” anasema Marwa.
Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard naye anaunga mkono hoja ya kutaka mgogoro uliopo utatuliwe haraka ili wananchi wa kata hiyo warudishe mahusiano na ujirani mwema na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Kiujumla hakuna mwananchi anayekataa wawekezaji wa hoteli za kitalii huku, kwanza ni kwamba tumechelewa, Serengeti ni moja ya hifadhi kubwa Tanzania na Afrika. Tulishasema watu wa hifadhi waje tukae wasikilize wananchi tumalize mgogoro uliopo,” anasema Tiboche.
Aidha diwani huyo anakiri kuwa mgogoro huo umewakosesha wananchi wa kata hiyo maendeleo ikiwemo miradi ya kijamii kutoka TANAPA.
“Sisi tuko tayari mgogoro utatuliwe lakini Serikali isimamie pande zote mbili [wanavijiji na hifadhi] zisikilizwe. Mgogoro huu umesababishia wananchi wangu hasara, tunakosa mambo mengi kutokana na kukosekana kwa ujirani mwema na hifadhi.
“Tungependa kuona hifadhi ikitujengea madarasa, zahanati na miradi mingine ya kijaamii isaidie wananchi wetu. Sisi tuko tayari kupokea miradi kutoka hifadhini ili wananchi nao waone hifadhi ina manufaa kwao.
“Kwa hiyo ninachotaka kuthibitisha ni kwamba sisi tuko tayari kupokea miradi yoyote kutoka kwa ndugu zetu majirani zetu wahifadhi ili wananchi waone wema wao,” anasisitiza Tiboche.
Wazo la RC Mzee
Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee aliwataka wakazi wa vijiji hivyo ambavyo ni Kegonga na Nyandage kuona umuhimu wa kuruhusu uwekezaji wa hoteli na kambi za kitalii katika eneo hilo.
RC Mzee alitoa pendekezo hilo mara baada ya kutembelea eneo hilo, akifuatana na viongozi wa CCM mkoa na wilaya kwa lengo la kusuluhisha mgogoro kati ya wananchi na hifadhi hiyo bora Afrika.
Alitaka wananchi hao kutunza mlima huo badala ya kuendelea kuutumia kwa shughuli za kilimo cha kujikimu, akiwapa mfano wa jinsi upande wa nchi jirani umetumia mlima kama huo kwa shuguli za kitalii ili kujikwamua kiuchumi.
“Tuangalie majirani zetu, wao wameruhusu kufanya shughuli za kitalii na kwa hiyo wanapata pesa. Sasa sisi tutafanyaje shughuli za kitalii wakati tunalima pale badala ya kuweka camp sites?
“Hapa nyie ni matajiri lakini mnajiletea umasikini wenyewe, hapa ambapo kuna nyumba zingejengwa hoteli za kitalii mngekuwa matajiri. Mnajikosesha utajiri,” alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Chandi akazia wazo
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi alikazia hoja hiyo ya kutenga milima hiyo kwa ajili ya uwekezaji wa kitalii na kuomba TANAPA) kupeleka wawekezaji wakubwa.
“Hii sehemu ni utajiri mkubwa, nashauri TANAPA ilete wawekezaji wakubwa ndani ya kijiji hiki wajenge hoteli katika milima hii - serikali ya kijiji ikusanye hela, kila mzungu akiingia analipa Dola nyingi, mtajikuta mnapata fedha nyingi, hili eneo tulifanye la uwekezaji,” alisema Chandi.
Akisisitiza zaidi uwekezaji huo, Chandi alitolea mfano kijiji cha Natta kilichopo wilaya jirani ya Serengeti - akisema kina milima miwili midogo kuliko iliyopo Nyanungu, ambayo imejengwa hoteli za kitalii zinazokiingizia mamilioni ya fedha kila mwaka.
Msindai aeleza umaarufu
wa eneo la Lamai
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Izumbe Msindai anasema eneo la hifadhi hiyo linalopakana na vijiji vya Kegonga na Nyandage katani Nyanungu ni muhimu kwa uhifadhi wa wanyamapori adimu na maarufu kwa utalii.
Msindai anasema eneo hilo linalojulikana kama Lamai na kwa jina jingine Kuinungu, ni muhimu zaidi kwa uendelevu wa ikolojia ya Serengeti, kwa mujibu wa tafiti za kisayansi.
“Mwaka 1960 tafiti za kisayansi zilifanyika zikaonesha eneo hilo ni muhimu sana kwa ikolojia ya Serengeti na hasa ukizingatia kwamba misafara ya wanyama wahamao maarufu kama nyumbu wanatumia muda mwingi kukaa kwenye eneo hilo la Lamai kwa sababu vyanzo vingi vya mito vinapatikana huko.
“Lakini pia mto maarufu wa Mara unapita sehemu hiyo ya Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na unawezesha wanyama hao kupata maji kwa mtumizi yao ya kila siku,” anasema Msindai.
Anaongeza kuwa tafiti za kisayansi zilizofanyika zinaonesha kuwa nyumbu wakikosa maji kwa muda wa siku tatu mfululizo wanakufa kwa wingi - kwa idadi ya kati ya laki tatu mpaka laki nne na nusu kwa siku.
“Kwa maana hiyo unaona kwamba tukiwapoteza wanyama hawa, kwa kiasi kikubwa Hifadhi ya Serengeti itapoteza umaarufu wake,” anasema Msindai.
Aidha Mkuu huyo wa Hifadhi anasema eneo la Lamai linafaa sana kwa uwekezaji wa kitalii kwa sababu wanyamapori adimu wanapatikana huko karibu mwaka mzima, lakini pia kipindi cha karibu miezi sita wanyama wahamaji (nyumbu) wanakuwa maeneo hayo.
Zaidi ya hapo, Msindai anasema ukienda juu ya eneo la Lamai kuna milima ya Isurya ambapo ukisimama kwa juu unaiona Hifadhi ya Serengeti kwa uzuri na ujumla wake. Hivyo linafaa sana kujenga hoteli kubwa za kitalii ambazo zitawezesha wageni [watalii] kuona vizuri eneo pana la ikolojia ya Serengeti.
Bahati nzuri Mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti anasema kwa sasa watu wengi wameonesha nia ya kuwekeza hoteli na kambi za kitalii kwenye maeneo hayo.
“Hivyo tunawashauri wananchi wa Nyanungu watumie eneo kinga (buffer zone) linalopakana na hifadhi hii kwa ajili ya uwekezaji ili waweze kukuza kipato chao kiuchumi.
“Tungependa kuona wananchi hao na wa vijiji vingine vilivyopo kando kando ya Hifadhi ya Serengeti upande wa Kaskazini katika wilaya ya Tarime wanabadilisha fikra na uelewa ili waweze kutumia fursa ya maeneo yao kwa uwekezaji, na tunatumaini yatawanyanyua zaidi kiuchumi,” anasema Msindai.
Anasema vurugu zinazofanywa na baadhi ya wananchi hivi sasa za kujaribu kutotambua mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ulioanzishwa kisheria mwaka 1968 hazina manufaa yoyote kwa jamii iishio pembezoni mwa hifadhi hiyo.
“Kwa hiyo niwaombe wananchi waheshimu sheria iliyoanzisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na waache kuvamia maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kilimo na ufugaji, ambazo zinamnufaisha mtu mmoja mmoja. Hifadhi hii ni yetu sote na iko kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo,” anasema Msindai.
Chanzo: SAUTI YA MARA
No comments:
Post a Comment