NEWS

Tuesday 9 May 2023

DC Mntenjele aipatia Shule ya Msingi Mtingiro msaada wa madawati 31



Na Mara Online News
-----------------------------------

MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ameipatia Shule ya Msingi Mtingiro msaada wa madawati 31 yenye thamani ya shilingi milioni mbili.

DC Mntenjele alikabidhi madawati hayo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Steven Rhobi shuleni hapo jana, ikiwa ni siku chache baada ya mwalimu huyo kumwomba msaada huo.

DC Mntenjele (kulia) waliokaa kwenye dawati, walimu, wanafunzi na viongozi wengine wakifurahia jambo wakati wa makabidhiano wa msaada huo wa madawati.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia nafsi hiyo pia kutoa wito kwa wadau wengine zikiwemo taasisi, kampuni na mashirika binafsi kujitokeza kuzipatia shule misaada ya aina hiyo ili kuzipunguzia changamoto.


“Nitoe wito kwa watu wengine wasamaria wema, taasisi, jumuiya na hata taasisi binafsi nao wajitahidi watusaidie kwa namna moja au nyingine kutupunguzia mzigo huu wa upungufu wa madawati katika shule zetu,” alisema.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa madawati, Mwalimu Rhobi alimshukuru DC Mntenjele, akisema umepunguza tatizo la upungufu wa madawati linaloikabili shule hiyo iliyopo kata ya Ketare katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara.

Sehemu ya msaada wa madawati uliotolewa na DC Mntenjele

Mwalimu Rhobi alisema hadi sasa shule hiyo ina uhitaji wa madawati 350, wakati yaliyopo ni 244 na upungufu ni 106.

Kwa upande wake, Afisa Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mwalimu Matiko Kabeha alitoa wito kwa viongozi, wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni ili kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages