Na Mara Online News
-----------------------------------
MAKUMI ya magari ya abiria na mizigo yamekwama kuvuka mto Tigithe (pichani juu) kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ambazo zimesababisha maji kufurika hadi juu ya daraja la mto huo eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Mara.
Taarifa zilizoifikia Mara Online News hivi punde kutoka eneo la tukio zinasema hali hiyo imetokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa muda wa nusu saa mfululizo jioni hii, na kwamba madereva wa magari hayo walikuwa wanaendelea kusubiri maji yapungue waweze kuvuka.
Magari yaliyokwama katika eneo hilo ni yaliyokuwa yanatoka Arusha, Serengeti na Nyamongo kwa upande mmoja, na yaliyokuwa yanatoka Tarime kuelekea Nyamongo, Serengeti na Arusha kwa upande mwingine.
Kutokana na hali hiyo, abiria na madereva wa magari hayo wameiomba Serikali kujenga daraja kubwa la kisasa katika eneo hilo ili kuepusha usumbufu kama huo wakati wa mvua.
Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwasiliana na mamlaka husika serikalini ili kujua hatua zinazochukuliwa kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
#Tunakuhabrisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment