NEWS

Friday, 17 April 2026

Mahafali Kidato cha Sita 2026 Mogoto Sekondari: CPA Magoti awapa wahitimu mbinu ya ushindi



Mgeni rasmi, CPA Lucas Magoti, akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Magoto, wakati wa mahafali ya 11 ya kidato hicho shuleni hapo jana.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
---------------

Wanafunzi wanaoelekea kuhitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Magoto iliyopo wilayani Tarime, mkoani Mara wamehimizwa kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mtihani wa taifa ujao.

Ushauri huo ulitolewa na CPA Lucas Magoti kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Tawi la Mwanza, wakati akizungumza katika Mahafali ya 11 ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo jana Aprili 16, 2026.

Katika hotuba yake, CPA Magoti alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kujituma katika masomo, kuzingatia nidhamu na kutumia muda vizuri ili kufikia malengo yao ya kitaaluma.
CPA Magoti akizungumza katika mahafali hayo

Kwa upande mwingine, CPA Magoti aliahidi kuipatia shule hiyo msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni moja ili kukuza vipaji vya michezo na kuimarisha afya kwa wanafunzi.

Aidha, aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ili kusaidia kupunguza na ikiwezekana kutatua kabisa changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo.

Miongoni mwa mahitaji ya shule hiyo ni maktaba ya kisasa, jiko la kisasa, nishati ya umeme jua (sola) na miundombinu bora ya kuvuna maji ya mvua ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
CPA Magoti na mwanafuzi wakikata keki

Akizungumza kwa niaba ya wenzake 84, mmoja wa wahitimu wa kidato cha sita katika shule hiyo, Anthony Stephano, alisema wamejipanga kikamilifu na wako tayari kuonesha matokeo yatakayoiwakilisha vyema shule yao.

Mtihani wa Taifa wa Kitado cha Sita unatarajiwa kufanyika nchini Mei mwaka huu.
Mgeni rasmi, CPA Lucas Magoto, walimu, ageni waalikwa na wanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Magoto katika picha ya pamoja.
Mgeni rasmi, CPA Lucas Magoti (kulia mbele), wakati wa mapokezi yake alipowasili shuleni hapo. (Picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages