
Shughuli za uokoaji wananchi waliozingirwa na mafuriko katika eneo la Mashambani kijijini Matongo.
Kikosi cha Dharura na Uokoaji (ERT) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kimesaidia kuokoa watu 22 wakiwemo watoto - waliokuwa wamezingirwa na mafuriko na kukwama kwa siku mbili katika kijiji cha Matongo, wilayani Tarime.

“Tulijitahidi kuokoa maisha yao wote waliokuwa wamezingirwa na maji na hakuna kifo wala majeruhi. Kwa hivyo, lazima tuwashukuru watu wa mgodi walifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na timu ya uokoaji ya wilaya na mkoa,” Meja Gowele aliwambia waandishi wa habari jana.
Shughuli za uokoaji zilianza Jumamosi iliyopita saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni katika eneo la Mashambani lenye makambi ya wakulima na wafugaji.
Baada ya kuokolewa, wananchi hao walipatiwa huduma ya kwanza na kusaidiwa kurejea kwenye makazi yao katika vijiji mbalimbali wilayani Tarime.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, alimshukuru Mkuu wa Wilaya, Gowele na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuchukua hatua za haraka kuokoa watu hao baada ya kuwapa taarifa za tukio hilo.
Ryoba alizishukuru pia timu za uokoaji za wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa kujitokeza kushiriki kuokoa maisha ya wananchi hao bila kukata tamaa.
Eneo la Mashambani kijijini Matongo lipo jirani na Mto Mara ambao unatiririsha maji kwenye Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwataka wananchi kuhama kutoka mabondeni, hasa misimu ya mvua nyingi.






No comments:
Post a Comment