Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda.
------------------------------------------
Na Mwandishi
Wetu, Musoma
----------------------
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda leo ametoa taarifa ya uandikishaji na mapokezi ya wanafunzi wa Darasa la Awali, Darasa la Kwanza na Kidato cha Kwanza hadi kufikia Januari 17, 2024 na kuzipongeza wilaya ya Musoma kwa kufanya vizuri.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Musoma leo Januari 18, 2024, RC Mtanda amesema taarifa zinaonesha kuwa Wilaya ya Musoma kupitia Halmashauri zake za Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma zimefanya vizuri katika uandikishaji na mapokezi ya wanafunzi hao.
“Ninaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa kuongoza kimkoa katika kuandikisha wanafunzi wa Darasa la Awali na Kidato cha Kwanza, na Manispaa ya Musoma kwa kuongoza katika kuandikisha wanafunzi wa Darasa la Kwanza,” amesema.
Kiongozi huyo wa mkoa amewataka viongozi wa wilaya, halmashauri, watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanafunzi wote waliotarajiwa kuanza masomo kwa mwaka 2024 wanapelekwa shule na wanaanza masomo.
“Nitoe wito kwa wakuu wa wilaya na viongozi wa ngazi zote kuhakikisha wanafanya msako wa wanafunzi wote wanaotakiwa kwenda shule wanaanza masomo kabla ya mwisho wa muda wa kupokea wanafunzi kwa mwaka 2024,” amesema RC Mtanda.
Aidha, amewapongeza viongozi wote, wasimamizi wa elimu, walimu wakuu na wakuu wa shule kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza masomo wanaanza masomo bila vipingamizi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara - Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bulenga Makwasa imeeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeandikisha wanafunzi 9,212 ambapo kati yao wavulana ni 4,692 na wavulana ni 4,520 sawa na asilimia 96.56 ya watoto 9,540 waliotarajiwa kuandikishwa Darasa la Awali.
Halmashauri nyingine zilizofanya vizuri uandikishaji wa Darasa la Awali ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti iliyoandikisha kwa asilimia 95.81 na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama (asilimia 91.99).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma pia imefanya vizuri katika uandikishaji wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, ambapo imeandikisha wanafunzi 4,092 kati ya wanafunzi 5,733 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari katika halmashauri hiyo ambayo ni sawa na asilimia 71.
Halmashauri nyingine zilizofanya vuzuri uandikishaji wa Kidato cha Kwanza ni Manispaa ya Musoma (asilimia 69.36) na Halmashauri ya Mji wa Bunda (asilimia 62.13).
Aidha, taarifa hiyo imeonesha kuwa Manispaa ya Musoma imefanikiwa kuandikisha wanafunzi 4,482 Darasa la Kwanza kati ya maoteo ya kuandikisha wanafunzi 4,437 kwa mwaka 2024 ambayo ni sawa na asilimia 101.01.
Halmashauri nyingine zilizofanya vizuri katika uandikishaji wa Darasa la Kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (asilimia 99.81), Halmashauri ya Wilaya ya Rorya (asilimia 96.18). Uandikishaji wa wanafunzi unaendelea hadi March 31, 2024.
No comments:
Post a Comment