NEWS

Tuesday 30 April 2024

Bodi ya Maji yatoa tahadhari ya mafuriko Bonde la Ziwa Victoria



Sehemu ya Ziwa Victoria mkoani Mara
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Mwanza
---------------------------------------------


BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imewataka wananchi wanaoishi na kujishughulisha karibu na vyanzo vya maji ndani ya bonde hilo kuchukua tahadhari juu ya ongezeko la maji.

Tahadhari hiyo inawalenga watumiaji wote wa maji wanaoishi karibu na vyanzo vya maji, wanaojishughulisha katika mialo na kando kando ya vyanzo vya maji na wenye miundombinu kwanye vyanzo vya maji.

“Utabiri unaonesha mvua zinaendelea kunyesha, hivyo kuna uwezekano wa maji kuongezeka zaidi,” ilieleza sehemu ya taarifa ya LVBWB kwa umma wiki iliyopita.

Ilifafanua kuwa kupitia vituo vya LVBWB vya ufuatiliaji, takwimu zimeonesha ongezeko la kiasi cha maji pamoja na ongezeko la mvua katika maeneo ya Kanda ya Ziwa katika kipindi cha robo hii ya mwaka, yaani kuanzia Januari hadi Machi, 2024.

“Kupitia vituo 70 vya kupima hali ya maji na mvua, takwimu zilionesha wastani wa mvua ni 124.2mm katika kipindi cha miezi mitatu (Januari- Machi), ambapo wastani wa muda mrefu kwa kipindi hiki ni 103.03mm,” ilifafanua.

Bodi hiyo ilitaja mambo manne yanayoakisi ongezeko la maji ndani ya bonde hilo kuwa ni wastani wa juu wa mvua, ongezeko la mtiririko wa maji katika mito, usawa wa maji katika mabwawa na ziwa pamoja na kupungua kwa uvukizi.

Bonde la Ziwa Victoria limegawanyika katika madakio matatu ya maji ambayo ni Dakio la Kagera lililopo magharibi, Dakio la Mara lililopo mashariki na Dakio la kati lililopo kusini mwa Ziwa Victoria.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages