NEWS

Wednesday 17 April 2024

Kinana amfagilia Prof Muhongo, asema ni mbunge mwenye maarifa na sio mpiga kelele



Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo (kulia) akimshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana kwa kutembelea jimbo hilo leo, ambapo ametumia nafasi hiyo pia kumweleza anavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM jimboni.
------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Musoma
---------------------------------------


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amemmiminia sifa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, akisema ni kiongozi mwenye maarifa, mchapakazi mahiri na anayesimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho ya Mwaka 2020-2025.

Amesema mbunge huyo ameonekana kuwa kinara wa kuweka maslahi ya wananchi mbele, hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kisekta ndani ya jimbo hilo, huku kila mradi ukiwa na ‘mkono’ wake.

Hadi sasa Musoma Vijijini ndilo jimbo pekee mkoani Mara lenye tovuti yake inayowezesha shughuli zake za maendeleo kuonekana dunia nzima.


Kinana akizungumza katika mkutano huo.
------------------------------------------------------

“Kama kuna jimbo linaenda kwa speed (kasi), ni Musoma Vijijini, kama treni ya umeme, mna mbunge mchapakazi, mwenye maarifa, sio mpiga kelele. Mkitaka jimbo liendelee, shikamaneni muwe na nguvu moja, msikubali kugawanywa na madalali maana ndio tabia yao wakiona watu wanaelewana,” amesema Kinana wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu na mabaraza ya jumuiya za CCM Musoma Vijijini leo mchana.

Kinana ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya hiyo kuimarisha mshikamano na kuepuka misuguanao.


Sehemu ya wajumbe mkutanoni.
-------------------------------------------

“Kamati ya siasa hamwelewani, mmeanzisha makundi yasiyo ya maana. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana, shule, zahanati, miradi ya maji na barabara inatekelezwa, na kuna uhuru wa kujieleza, hivyo hakikisheni tunapata ushindi mnono katika uchaguzi ujao,” amesema Kinana.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi akimkaribisha kiongozi huyo wa kitaifa kuzungumza na wajumbe hao, alisema hali ya CCM Musoma Vijijini ni shwani na kwamba changamoto ndogo ndogo zilizopo zinashughulikiwa kikamilifu.


Mwenyekiti Chandi akizungumza 
katika mkutano huo.
------------------------------------------------------

Aidha, Chandi aliwakumbusha wajumbe hao kushirikiana na wanachama wengine kujipanga na kuhakikisha wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM wanashinda kwa kishindo nafasi za uongozi wa vijiji na vitongoji wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Kinana, yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku tano ya kuimarisha chama hicho,.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages