Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Hamad Masauni.
--------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------
Serikali imeonya kuwa haitavumilia kuona mauaji ya wananchi, wala vitendo vya uvamizi na uporaji wa mali vikiendelea katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
“Serikali haifurahii kuona wananchi wake wanakufa na kuumia, lakini pia haifurahii kuona wawekezaji ambao wanafanya kazi zao kihalali wanavamiwa na mali zao zinaporwa, yote haya ni mambo ambayo hayakubaliki,” Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameonya.
Waziri Masauni alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Nyamichele, kilomita chache kutoka mgodi wa North Mara wilayani Tarime, jana Alhamisi.
“Tumetoa maelekezo kwa askari [polisi] kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi zaidi, wanaotekeleza majukumu yao kinyume na sheria wachukuliwe hatua,” aliagiza.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
---------------------------------------------------
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema serikali inafanyia kazi ombi la wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo la kuwatengea wachimbaji wadogo maeneo na kuwawezesha vitendea kazi vya kisasa.
“Tumekaa pamoja na mgodi na tumewapa maelekezo, maeneo ambayo tutakubaliana kutenga yatapata leseni," Waziri Masauni aliwambia wananchi na kuongeza:
“Pia nimeelekeza STAMICO watakuja hapa kusaidia uchorongaji ili uchimbaji uwaongezee tija kiuchumi kuliko sasa hivi ambapo asilimia kubwa mnachimba kwa kubahatisha.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alisema dhamira ya serikali ni kuona wananchi wanapiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Kama mkoa tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wana-Mara wanatoka hapa walipo kwenda hatua nyingine, tuache tabia ya kwenda kule [kuvamia mgodi], yajayo yanafurahisha,” alisema Kanali Mtambi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Kanali Evans Mtambi.
---------------------------------------------------------
Awali, wananchi waliwaomba viongozi hao kusaidia utatuzi wa migogoro ya muda mrefu ikiwemo ya fidia kwa wanaohamishwa kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara.
Aidha, wananchi hao waliwadokeza viongozi hao kwamba migogoro iliyopo inachangiwa na viongozi wachache kwa maslahi yao binafsi.
Sehemu ya wananchi katika mkutano huo.
---------------------------------------------------
Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Rashid alisema matatizo yaliyopo yanahitaji ushirikiano wa serikali na wananchi katika kuyatatua bila kusababisha madhara.
“Mgodi si kwamba hauna faida kwa wananchi, ila tatizo kubwa ni hawa vijana kukosa maeneo ya uchimbaji kwa ajili ya kujipatia riziki. Lakini pia maeneo yao ya uchimbaji yanahitaji umeme na barabara,” alisema Bogomba.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
No comments:
Post a Comment