NEWS

Wednesday 10 July 2024

Mtanzania Bhoke Nyambari Nyangwine ang’ara Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza



Bhoke Nyambari Nyangwine akifurahia zawadi katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------

Hatimaye kipindi cha miaka mitatu ya kazi ngumu ya kusoma na kuwajibika kimezaa matunda, na leo binti anajionea fahari ya kuwa msomi mwenye digrii adhimu ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, nchini Uingereza.

Binti huyu si mwingine, bali ni Bhoke Nyambari Nyangwine (21), mzaliwa wa Tanzania ambaye wiki hii amehitimu Digrii ya Sheria (Bachelor of Laws with Honors, First Class) huku akijivunia kupata daraja la kwanza.

Bhoke ambaye anasema alitumia muda wake mwingi kuhakikisha anatimiza lengo lake la kufanya vizuri darasani, alifanikiwa kufaulu vizuri huku akiwa Mwafrika pekee katika darasa lililokuwa na wanafunzi 80 katika chuo hicho ambacho ni moja ya vyuo bora nchini Uingereza.
Bhoke (wa pili kushoto) akifurahia picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wenzake.
--------------------------------------------------

“Niliweka starehe zote kando na kujali zaidi masomo. Nilitaka kuwa mfano bora wa kuigwa na wasichana wengine,” alisema Bhoke mara baada ya mahafali yake mwaka huu.

Anawashukuru wazazi wake kwa kumgharimia masomo yake nchini Uingereza, hasa baba yake Nyambari Nyangwine, na kutoa wito kwa wazazi wengine na hata mashirika ya misaada kujitolea kugharimia elimu ya mtoto wa kike.

“Sina shaka kuna wasichana wengi wenye vipaji katika nyanja mbalimbali. Leo mimi nimesoma sheria, lakini kuna wasichana wengine pia wana uwezo katika masomo ya sayansi na sanaa, wanahitaji tu kuwezeshwa,” anasema Bhoke.

Msichana Bhoke alisoma Shule ya Awali na Msingi Dar es Salaam Independent School (DIS), kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari DIS na kidato cha tano hadi cha sita katika DIS High School, kabla ya kwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza.

Bhoke ni mtoto wa kwanza wa familia ya Nyambari Nyangwine ambaye ni mfanyabishara, mwandishi na mchapishaji maarufu wa vitabu Tanzania.

Nyambari pia ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara mwaka 2010 hadi 2015.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages