NEWS

Saturday, 30 November 2024

Askofu Msonganzila amshukuru Nyambari Nyangwine kuhudhuria Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre wake



Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia nyekundu) akiwa katika sherehe za hitimisho la Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre wa Askofu Michael Msonganzila (aliyeweka mkono kifuani), zilizofanyika juzi Ukirigulu, Misungwi mkoani Mwanza.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Misungwi

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila amemshukuru mfanyabisha, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine kwa kuhudhuria hitimisho la Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre wake.

Sherehe za Jubilei hiyo zilifanyika juzi Novemba 29, 2024 katika kijiji anakotoka Askofu Msonganzila cha Ukirigulu kilichopo wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

Askofu Msonganzila alisema Nyambari ameonesha upendo na heshima kuhudhuria sherehe hizo ambazo zilifana kwa aina yake.

Sherehe hizo pia zilihuhduriwa na idadi kubwa ya maskofu na mapadre kutoka sehemu mbalimbali nchini, miongoni mwa wageni wengine.

Agosti 29, 2024, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan katika Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre wa Askofu Michael Msonganzila, iliyofanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) na Christopher Kangoye (katikati) wakiwa kwenye sherehe ya hitimisho la Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre wa Askafu Michael Msonganzila kijijini Ukirigulu juzi.
--------------------------------------

Nyambari Nyangwine amekuwa rafiki wa karibu wa muda mrefu wa Askofu Msonganzila, ambapo pamoja na mambo mengine amekuwa akishiriki katika maendeleo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma.

Mfano, Desemba 2023 Nyambari alikuwa mgeni ramsi katika harambee ambayo alichangisha shilingi milioni 320 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga iliyopo wilayani Tarime, mkoani Mara. Harambee hiyo ilifanyika sambamba na sherehe ya kumpongeza Askofu Msonganzila kwa kutimiza miaka 40 ya upadre.

Pia, Septemba 2024, Nyambari aliongoza harambee nyingine ambayo alichangisha shilingi milioni 224, ambapo Askofu Msonganzila alishiriki katika harambee zote mbili.
Askofu Michael Msonganzila akiwa na Nyambari Nyangwine (katikati) wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la Parokia ya Nyamwaga, Desemba 2023. Kushoto ni Mhariri wa Mara Online News, Christopher Gamaina.
---------------------------------------

Nyambari ambaye pia ni kada wa chama tawala - CCM, amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010 hadi 2015.

Hivi karibuni, mfanyabiashara na mwanasiasa huyo alianzisha Taasisi ya Nyambari Nyangwine (NNF) yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, ambapo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ally Khamis alimwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa kuizindua.

Miongoni mwa malengo ya Taasisi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshaji wa huduma za elimu na afya, kutengeneza ajira, kukukuza utamaduni wa Mtanzania kikanda na kimataifa, huku suala la lugha ya Kiswahili likipewa kipaumbele.

Kwa muda mrefu, Nyambari kupitia kampuni zake amekuwa akisaidia umma wa Watanzania katika sekta za elimu, afya, maji na kupeleka misaada muhimu ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Lengo kubwa la Nyambari Nyangwine Foundation ni kumsaidia Mtanzania kupiga vita umaskini. Umefika wakati kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na taasisi hii ili wapate ujuzi na maarifa. Kwenye ajira tutasisitiza suala la ujasiriamali kuhusu namna ya kijiajiri,” alisema Nyambari na kuongeza kuwa taasisi hiyo pia itaunga mkono juhudi za Serikali katika utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages