NEWS

Monday, 28 April 2025

Barrick yaimarisha afya na usalama migodini kupitia teknolojia mpya



Afisa wa Mgodi wa Bulyanhulu, Chrisant Maduhu (kulia), akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, kwenye Maonesho ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi katika viwanja vya Mandewa mjini Singida juzi.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Singida

Migodi ya Barrick na Twiga ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi inadhihirisha kwa vitendo kaulimbiu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya OSHA nchini mwaka huu isemayo “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia katika Kuimarisha Afya na Usalama Kazini” kutokana na kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa za kimataifa katika uendeshaji wa shughuli zake.

Katika Maonesho ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ambayo hufanyika kila mwaka na kuandaliwa na Wakala wa Afya na Usalama na mahali pa kazi (OSHA), ambapo mwaka huu yanayofanyika katika viwanja wa Mandewa mjini Singida.

Wananchi wengi na viongozi mbalimbali wanatembelea banda la maonesho la migodi ya Barrick na kujionea teknolojia za kisasa za kidigitali za kudhibiti majanga na kupata mafunzo ya kuhusiana na usalama mahali pa kazi na kwenye jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alipotembelea banda la migodi wa kampuni ya Barrick yenye ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga jana, alisema mitambo, magari ya kisasa, vifaa vya tekonolojia na kidigitali ni chachu ya mabadiliko ya utendaji kazi kwenye sekta ya uchimbaji wa madini kama ambavyo migodi ya Barrick inaendesha shughuli zake.

“Kwa kweli kwa matumizi ya digitali na akili mnemba migodi ya Barrick mnafanya vizuri katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi pamoja na jamii inayozunguka migodi. Hili ni jambo la kuungwa mkono kwa dhati na kuigwa na makampuni mengine katika sekta ya uchimbaji madini,” alisema Dendego.

Aliongeza kwamba ni muhimu kwa kuhakikisha usalama na afya za wafanyakazi kama vile migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara inavyowekeza katika teknolojia za kisasa ili kudhibiti madhara yatokanayo na ajali na majanga mengine kwenye sekta ya madini.

Akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa huyo, Mrakibu Mwandamizi wa Usalama, Meshack Issack kutoka Mgodi wa North Mara, alisema mgodi huo unatumia mitambo ya kisasa ya uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi na kuachana na matumizi ya binadamu katika uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi, hali ambayo inaleta usalama na afya kwa wafanyakazi.

“Tuna mashine za kisasa za teknolojia ya kimataifa (automation) ambazo zinaendeshwa na mfanyakazi akiwa ofisini lakini anachimba dhahabu chini ya ardhi ambayo inaweza kutambua hali hatarishi yoyote kwenye miamba na kuta za chini ya ardhi,” alieleza.

Isaack aliongeza kuwa mgodi huo umeachana uchimbaji wa kizamani ambapo Kwa sasa unatumia akili mnemba ambayo inarahisisha kazi na kuokoa muda na mfanyakazi wa mitambo hiyo ya kisasa anatumia rimoti katika ufanyaji wake wa kazi.

Kwa upande wake, kiongozi wa Usalama na Afya wa Mgodi wa Buzwagi, Dkt Ludovick Sirima, alisema mgodi huo upo kwenye hatua za ufungaji baada ya shughuli za uchimbaji dhahabu kuisha, lakini afya na usalama wa wafanyakazi ni kipaumbele chao.

“Pamoja na mambo mengine, mgodi wa Buzwagi unaendelea na jitihada za kuandaa kongamano maalum la uwekezaji ili kuhakikisha baada ya shughuli za ufugaji kuisha basi Watanzania wanapata fursa nyingine ya kibiashara na uwekezaji wa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi,” alisema Dkt Sirima.

Naye Mkufunzi wa Mafunzo na Usalama wa Mgodi wa Bulyanhulu, Chrisant Madubu, alisema mgodi huo unatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya akili mnemba mahali pa kazi kwa kuachana na matumizi ya karatasi na kuweka mifumo ya teknolojia na kidigitali kwa kuwa na mitambo na magari ya kisasa katika shughuli za uchimbaji.

"Kampeni yetu ya ‘Journey to Zero’ inalenga kuhakikisha wafanyakazi wote wa kampuni wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa kazini hadi wanaporudi nyumbani, na tumehakikisha kampeni hii inavuka mipaka hadi nje ya kampuni kuhakikisha jamii nzima inakuwa salama, ndio maana tunaendelea kutoa mafunzo ya usalama kwa jamii,” alisema Maduhu.

Mmoja wa wageni waliotembea mabanda ya migodi ya Barrick, John Lucas, mkazi wa Iyambi, Singida alisema amevutiwa jinsi mgodi unavyotekeleza sera ya afya na usalama sambamba na matumizi ya vifaa vya kisasa katika kudhibiti majanga.

"Usalama ni jambo la msingi, ni muhimu nasi wananchi tupatiwe elimu ya kukabiliana na majanga ili tubaki salama katika jamii," alisema Lucas.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages