NEWS

Friday, 25 April 2025

Katibu Mkuu CCM apiga marufuku wimbo unaobeza wapinzani



Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Shirati, wilayani Rorya leo Aprili 25, 2025. (Picha na Mara Online News)
------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Rorya

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, amekemea na kupiga marufuku video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha wanachama wa chama hicho tawala wakiimba wimbo unaohamasisha chuki dhidi ya wafuasi wa chama cha upinzani.

"Tunapita kwenye uchaguzi lazima vyama vipime kauli kulinda amani ya nchi yetu. Mimi kama Katibu Mkuu naupiga marufuku kuanzia leo," amesema Balozi Dkt Nchimbi wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Shirati, wilayani Rorya leo Aprili 25, 2025.

Aliongeza: "Tutoe kauli za kuunganisha kama baba na mama wa demokrasia, amani, umoja na mshikamano… tunataka nchi yenye mshikamano.”

Katibu Mkuu huyo wa CCM ametumia fursa hiyo pia kuwaomba viongozi wa dini kuepuka kauli za uchonganishi, badala yake wawe chachu ya kuwaunganisha Watanzania kwa kuwakumbusha viongozi wajibu wao kwa maslahi ya taifa.

Wananchi wakimpungia mikono katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wa hadhara mjini Shirati leo.
------------------------------------

Pia, alikagua soko la kisasa la Tarime na kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Serengeti “Shamba la Bibi”.

Ratiba inaonesha kuwa kesho Jumamosi, kiongozi huyo wa CCM Taifa ataelekea wilayani Serengeti kupitia mji mdogo wa Nyamongo ambapo atasimama kwa muda kusalimiana na wananchi.

Balozi Dkt Nchimbi anaendelea na ziara yake ya siku tano mkoani Mara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 na kuzungumza na wananchi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages