
Paul Chacha Makuri
Ndugu Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi,
Kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Serengeti na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tunapokea kwa furaha na shukrani kubwa ziara yako ya kikazi hapa Serengeti, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku tano mkoani Mara.
Katika kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ujio wako unakuja kwa wakati muafaka. Ni fursa ya Chama kusikiliza kwa karibu sauti ya wananchi na kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020–2025.
Aidha, tunakupa pongezi za dhati kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM. Heshima hii si yako binafsi tu, bali pia ni fahari kwa Watanzania wote.
Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita wilayani Serengeti:
Tunashukuru kwa mafanikio mbalimbali yaliyoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ikiwemo:
• Ujenzi wa vituo vya afya na Hospitali ya Wilaya
• Ujenzi wa shule mpya na maboresho ya miundombinu ya elimu
• Usambazaji wa umeme kwenye vijiji vingi
• Maboresho ya huduma za maji, afya na ustawi wa jamii
Hata hivyo, zipo changamoto ambazo bado zinahitaji msukumo wa ziada kutoka kwenye chama na kufanyiwa kazi na serikali kama ifuatavyo:
1. Miundombinu ya barabara:
• Wilaya ya Serengeti haijaunganishwa kwa barabara za lami na wilaya jirani kama Tarime, Bunda, na makao makuu ya Mkoa-Musoma.
• Kukosekana kwa barabara za uhakika kumeathiri usafirishaji wa mazao, huduma za afya, na utalii.
2. Huduma za afya:
• Baadhi ya vituo vya afya bado vina uhaba wa watumishi na vifaa tiba, hali inayokwaza utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
3. Elimu:
• Licha ya uwepo wa shule nyingi, changamoto ya upungufu wa walimu na vifaa vya kujifunzia bado ni kubwa katika shule zetu.
Wito kwa Chama Cha Mapinduzi:
Tunakuomba uone haya si tu kama maoni ya wananchi, bali ni kilio cha muda mrefu kinachohitaji hatua ya dhati. Tungependa changamoto hizi ziingizwe kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025–2030 ili kuhakikisha zinawekewa mipango madhubuti ya utekelezaji.
Hitimisho:
Karibu sana Serengeti, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi. Tunaamini ziara yako italeta mwanga mpya, kuhamasisha mshikamano, na kuimarisha matumaini ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu. Tuko pamoja nawe katika safari ya kuijenga Tanzania mpya kupitia CCM.
“Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”
Ndimi,
Paul Chacha Makuri,
Mdau wa maendeleo na kada wa CCM.
No comments:
Post a Comment