NEWS

Thursday, 1 May 2025

Rais Samia apandisha mshahara kwa wafanyakazi wa umma



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akipungia mkono wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida leo Mei 1, 2025.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Singida

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma kwa asilimia 35.1.

Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida leo Mei 1, 2025, Rais Samia amesema uamuzi huo umetokana na kuimarika kwa uchumi wa taifa - kutokana na juhudi kubwa za wafanyakazi.

"Baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda, na umepanda kwa sababu ya nguvu zenu wafanyakazi, nina furaha kuwatangazia kuwa mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1," amesema.

Rais Samia ameeleza kuwa nyongeza hiyo itaanza kutumika rasmi Julai mwaka huu, ambapo kima cha chini cha mshahara kitaongezeka kutoka shilingi 370,000 hadi 500,000.

Aidha, amesema mishahara kwa ngazi nyingine pia itapanda kwa viwango tofauti kutegemeana na uwezo wa bajeti ya serikali.

“Ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa kiwango kizuri jinsi bajeti inavyoruhusu, lakini nataka niwambie nyongeza nzuri ipo,” amesema.

Kwa upande wa sekta binafsi, kiongozi huyo wa nchi amesema Bodi ya Kima cha Chini cha Mshaharaa inaendelea kufanya mapitio ili kuboresha viwango vya chini vya mshahara kwa wafanyakazi wa sekta hiyo.

“Pamoja na kazi inayofanywa na bodi hiyo, naendelea kuvihimiza wizara na vyama vya wafanyakazi, kufanya majadiliano na waajiri ili kutekeleza mikataba ya hali bora ya wafanyakazi katika sekta binafsi waendane sambamba na wenzao wa sekta ya umma.

“Ahadi yetu kwenu wafanyakazi ni kwamba tutaendelea kuboresha mazingira ya kazi, yakiwemo maslahi ya wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu,” amesema Rais Samia.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya wafanyakazi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages