NEWS

Monday, 1 December 2025

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane kuzindua Birth Day ya simba




Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George (katikati waliokaa) akizungumzia tukio lijalo la Birth Day ya simba katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani).


Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane inawaalika na kuwakaribisha watalii kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio la kihistoria la 'Birth Day' ya miaka 10 ya simba katika hifadhi hiyo.

Sherehe hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kufanyika nchini, itazinduliwa Desemba 20, 2025 ndani ya hifadhi hiyo iliyopo katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, sherehe hiyo itahusisha matukio ya kuwaona mbashara simba husika wakilishwa keki pamoja na kupata simulizi za kusisimua kuhusu tabia, maisha na umuhimu wa wafalme hao wa pori katika utalii na uhifadhi.

"Lengo la tukio hili la uzinduzi wa Birth Day ya simba ni kuongeza hamasa ya utalii katika hifadhi yetu ya Kisiwa cha Saanane," amesema Dkt. Tutindaga katika mkutano na waandishi wa habari hifadhini hapo leo Desemba 1, 2025.

Ameongeza kuwa Birth Day hiyo ya simba imeandaliwa ili kuenzi umaarufu wa wanyamapori hao, ambao licha ya kuwa wakali, jasiri na mahiri katika kuwinda, wameendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo muhimu cha mapato kwa taifa kupitia sekta ya utalii.
Mmoja wa simba wanaohifadhiwa katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane

Dkt. Tutindaga amebainisha kuwa sherehe hiyo ni mahsusi kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo na makundi mengine ya jamii kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Kwa upande wake Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka Kitengo cha Utalii, Pellagy Marandu, amesema Birth Day hiyo pia itaambatana na matukio ya wanafunzi kuulizwa maswali na washindi kupewa zawadi mbalimbali, yakiwemo mabegi yenye picha ya simba na nembo ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.

Simba ni moja ya wanyamapori maarufu katika kundi la Big Five ambao ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini .

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo na waandishi wa habari ni Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyamapori, Anifa John, Daktari Msaidizi wa Wanyamapori, Andrea Idrissa Mbwambo na Mwalimu Gilbert Tindabatangile kutoka Shule ya Sekondari Mkolani, jijini Mwanza.





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages