NEWS

Wednesday, 20 May 2026

Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mara laanika mafanikio lukuki



Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila (aliyekaa kiti cha dereva), akifurahi wakati wa kukabidhi matrekta matatu kwa vyama vya ushirika, mara baada ya kufungua mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara wilayani Serengeti jana.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
--------------

Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara limeweka wazi mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia vyama vya ushirika na hivyo kuchochea maendeleo ya kilimo katika mkoa huo wa Kanda ya Ziwa.

Mafanikio hayo ni pamoja na uwekezaji wenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 28 ambao umewezesha kutoa fursa mbalimbali za ajira za kudumu na za msimu zipatazo 408.

Hayo yalielezwa kwenye risala ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara kwa mgeni rasmi, iliyosomwa na Samwel Gisiboye katika mkutano wa siku mbili wa Jukwaa hilo ulioanza wilayani Serengeti jana.

Gisiboye aliongeza kuwa kupitia vyama vya vshirika katika msimu wa 2025/2026, wameweza kusambaza kwa wakulima pembejeo za kilimo tani 622. 35 zenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 810 ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati.

Gisiboye akizungumza katika mkutano huo

“Pia tumeweza kusambaza miche bora ya kahawa ipatayo 500,000 ambapo Rorya DC wamesambaziwa miche 43,000, Butiama DC miche 44,000, Tarime TC miche 80,000, Tarime DC miche 268,000 na wakulima binafsi wamechukua miche 65,000.

“Mazao mbalimbali yenye uzito wa kilo 10,788,394.56 na thamani ya shilingi 18,916,648,509 yamekusanywa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika, hivyo kuchangia shilingi 617,053,495.08 kwa serikali kupitia tozo mbalimbali.

“Hadi Machi 2026, vyama vya ushirika wa kifedha vilikuwa vinamiliki Dhima (Hisa; Akiba & Amana) yenye thamani ya shilingi 8,458,514,635 na kuwezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya shilingi 9,038,571,741,” alisema Gisiboye.

Alifafanua kuwa hali hiyo imechochea shughuli za kiuchumi na ajira, hivyo kuinua pato la taifa kupitia tozo mbalimbali zinazolipwa na wajasiriamali wanaopata mikopo husika.

“Katika mwaka 2025, vyama vya ushirika vimechangia shilingi 8,590,000, ikiwa ni misaada ya aina mbalimbali kwa maendeleo ya kijamii,” aliongeza Gisiboye ambaye ni Mjumbe wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara.

Hata hivyo, Kusaya alisema Jukwaa hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo madeni makubwa kwa vyama vikuu yaliyotokana na makabidhiano ya mali za iliyokuwa Mara (1984) Coop, hivyo kuwa kikwazo kwa maendeleo ya sekta ya ushirika katika mkoa huo.

Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, alivielekeza vyama vya ushirika kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwasaidia wanaushirika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kuboresha mawasiliano na ufanisi wa shughuli zao.

Vilevile, alikielekeza Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) na wadau wa sekta ya ushirika kuimarisha programu za mafunzo ya kitaalamu ili kuwapa viongozi na wanachama ujuzi unaohitajika katika matumizi ya TEHAMA.

RAS Kusaya akizungumza katika mkutano huo

Aidha, Kusaya alilielekeza Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara mkuhakikisha linakuwa na mipango madhubuti ya kuendeleza na kuimarisha vyama vya ushirika katika misingi ya usimamizi na uwekezaji wenye tija.

“Ninaviagiza vyama vya ushirika kuweka mikakati stahiki ya uwekezaji wenye tija ambao utaviimarishia uwezo wa kukidhi mahitaji ya wanaushirika kiuchumi na kijamii,” aliagiza.

Alihimiza viongozi wa vyama vya ushirika na wadau wa sekta ya ushirika kuendelea kuhamasisha wananchi, hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujiunga na vyama hivyo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji na kuhimili ushindani wa kiuchumi.

Sambamba na hilo, Kusaya aliwataka viongozi wa vyama vya ushirika kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria za ushirika na taratibu za fedha ili kuepuka migogoro na upotevu wa rasilimali za vyama hivyo.

“Aidha, mnapoelekea kwenye mwaka wa uchaguzi wa vyama vya ushirika, niwatake kusimamia kisingi ya sheria ili kuwezesha upatikanaji wa viongozi watakaojenga taswira ya ushirika iliyosimama kibiashara na kutaleta tija kwa wanaushirika,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, RAS Kusaya aliitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha uwepo wa mifumo thabiti ya kutoa mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum ili nao waweze kunufaika fursa za ushirika.

Katibu Tawala huyo wa mkoa wa Mara alitumia nafasi hiyo pia kukabidhi matrekta matatu mapya kwa vyama vya ushirika kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha kilimo cha mzao mbalimbali.

Matrekta yaliyokabidhiwa kwa vyama vya ushirika. (Picha zote na Sauti ya Mara)

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages