
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serngeti, Ayub Mwita Makuruma, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani jana.
Serengeti
----------------
Maadalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti yameiva, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara limeelezwa.
Akizungumza katika kikao cha baraza hilo wilayani Serengeti jana, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma, alisema tayari serikali imeanza rasmi hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
"Suala la uwanja wa ndege limepata mwafaka kwa msaada wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mbunge peleka salaam, tunafurahi mambo yanavyoendelea, hivi karibuni timu maalum inakuja Serengeti kuhakikisha ujenzi unaenda kuanza,” alisema Makuruma.
Ujenzi wa uwanja huo umekuwa ukisubiriwa kwa miaka mingi ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii kupitia utalii katika wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara.
Kikao hicho cha madiwani kilikuwa cha kupokea taarifa za maendeleo kutoka katika kamati za halmashauri hiyo, taasisi na mashirika ya serikali.
Pia, yalitolewa madawati yenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya Shule ya Msingi Kambarage na saruji mifuko 2,597 zitakazogawanywa kwa kata 30.
"Mary ameanza vizuri, historia itamkumbuka, umeleta cement (saruji), madawati ya milioni mbili kukamilisha Zahanati ya Kisala,” alisema Makuruma na kuongeza:
"Waheshimiwa madiwani, mwenzetu muda umeanza kumtetea na sisi tunapaswa kuwa hapo, vifaa hivi viende vikafanye kazi iliyokusudiwa.”
Naye Mbunge Mary ambaye pia ni mjumbe wa baraza hilo la madiwani, alitumia fursa hiyo kuwataka madiwani kuhakikisha wanasimamia vifaa hivyo ili vitumike kama ilivyokusudiwa katika kuboresha na kukamilisha miundombinu ya huduma za kijamii katika kata zao.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kambarage wakifurahia madawati yaliyotolewa na Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Serengeti.Katikati waliokaa ni Mbunge Mary Daniel Surati na wa kwanza kulia waliokaa ni Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema. (Picha zote na Mara Online News)



No comments:
Post a Comment