NEWS

Thursday, 21 May 2026

Prof. Muhongo achaguliwa Makamu wa Rais wa Baraza la Uongozi la Akademia ya Sayansi Afrika



Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na mwanazuoni maarufu nchini, Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Uongozi la Akademia ya Sayansi ya Bara la Afrika (AAS) kwa Nchi za Mashariki Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu (2026-2029).

Akademia hiyo inajumuisha wanasayansi wabobezi wa fani mbalimbali wapatao 676 barani Afrika.

Taarifa kutoka ofisi ya mwanazuoni huyo imeeleza kuwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa njia ya kielektroniki yanaonesha kuwa kura za "Ndiyo" alizopata Prof. Muhongo ni 168, kura za "Hapana" ni mbili na kura za "Kujizuia" ni 15, huku asilimia ya kura zilizopigwa ikiwa 74.60.

Prof. Muhongo ni msomi mwenye wasifu ulioshiba anayetambulika kimataifa kama mwanasayansi maarufu. Ana shahada ya udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin, Ujerumani.

Hapa Tanzania amewahi kushika wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Chama cha Jiolojia Afrika na Mwanachama wa Akademia ya Sayansi Bara la Afrika.

Pia, ni Mwanachama wa Heshima wa Vyama vya Jiolojia vya London na Marekani na Mtafiti wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Jiolojia cha China.

Hali kadhalika, Prof. Muhongo alikuwa Mkurugenzi wa Kanda Mwanzilishi wa Afrika wa Baraza la Kimataifa la Umoja wa Vyama vya Sayansi (ICSU).

Pia, msomi huyo ni Mhariri Mkuu wa Jarida la African Earth Sciences, Elsevier, na Makamu wa Rais wa Tume ya Ramani ya Jiolojia ya Dunia (CGMW).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages