
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati (wa pili kushoto), akigawa sehemu ya saruji mifuko 2,597 katika hafla iliyofanyika jimboni humo, Mei 20, 2026.
Akiripoti kutoka
Serengeti
--------------
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, ameendelea kuweka historia ya maendeleo katika jimbo hilo baada ya kutoa na kugawa shilingi milioni 88 kwa ajili ya miradi ya huduma za kijamii.
Mary alitoa fedha hizo kupitia Mfuko wake wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, katika hafla maalum iliyofanyika Mei 20, 2026 wilayani Serengeti na kuhudhuriwa na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, viongozi wa serikali na wananchi.
Mbunge huyo alisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wa Serengeti wanapata huduma bora za afya, elimu na maendeleo ya kijamii kwa ujumla.
Katika mgao huo wa fedha, kiasi cha shilingi milioni 25 kimetengwa kwa ajili ya kugharimia ukamilishaji wa Zahanati ya Kisaka, mradi unaotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo na kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Mbunge Mary akikabidhi hundi ya mfano ya milioni 25/-
Mbali na fedha hizo, Mbunge Mary pia alikabidhi madawati kadhaa yenye thamani ya shilingi milioni mbili ambayo yalielekezwa Shule ya Msingi Kambarage pamoja na mifuko 2,597 ya saruji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata 29 za jimbo hilo.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya kijamii katika maeneo mbalimbali jimboni.
Katika kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo, Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation) ilichangia saruji mifuko 500 iliyogawiwa kwa kata mbalimbali ndani ya jimbo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge Mary aliwataka madiwani kuhakikisha wanasimamia vifaa hivyo ili vitumike kama ilivyokusudiwa katika kuboresha na kukamilisha miundombinu ya huduma za kijamii katika kata zao.
Alisema maendeleo ya wananchi yanahitaji mshikamano wa viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo, huku akiahidi kuendelea kutumia nafasi yake ya ubunge kuhakikisha Serengeti inapiga hatua katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kambarage wakifurahia madawati yaliyotolewa na Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Serengeti. Katikati waliokaa ni Mbnunge Mary na wa kwanza kulia ni Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema. (Picha zote na Mara Online News)
Baadhi ya madiwani waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma, walimpongeza mbunge huyo kwa kuendelea kuelekeza nguvu katika miradi yenye manufaa kwa wananchi.
"Mary ameanza vizuri, historia itamkumbuka, umeleta cement (saruji), madawati ya milioni mbili kukamilisha Zahanati ya Kisaka,” alisema Makuruma na kuongeza:
"Waheshimiwa madiwani, mwenzetu muda umeanza kumtetea na sisi tunapaswa kuwa hapo, vifaa hivi viende vikafanye kazi iliyokusudiwa.”
Kwa upande wao, wakazi wa jimbo la Serengeti wameonesha matumaini wakisema fedha na vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuwezesha maboresho katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment