NEWS

Thursday, 28 May 2026

Sagini achinja ng'ombe 400, kondoo 1,000 Sikukuu ya Eid Al-Adha, agawa nyama kwa wananchi



Jumanne Abdallah Sagini (kushoto mbele) akikagua sehemu ya ng’ombe walioandaliwa kwa ajili ya kuchinjwa.

Na Mwandishi Wetu
Butiama
--------------

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Butiama, Jumanne Abdallah Sagini, kwa kushirikiana Taasisi ya ITTIFAK International kutoka nchini Uturuki, amechinja ng'ombe 400 na kondoo 1,000 na kugawa nyama kwenye vitongoji 370 na taasisi zote za umma na binafsi zilizopo katika wilaya za Butiama na Musoma, mkoani Mara kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi kusherehekea Sikukuu ya Eid Al-Adha.

Tukio hilo la sadaka limefanyika Mei 27, 2026 nyumbani kwa Sagini katika kijiji cha Kiabakari, kata ya Kukirango wilayani Butiama, kama sehemu ya kuimarika kiimani, ukarimu. mshikamano na upendo.

Sheikh wa Kata ya Mugango iliyopo jimbo la Musoma Vijijini, Mwabadi Yusuph Chogero, alisema kipindi hiki Sagini amepanua wigo zaidi kwani sadaka hiyo imewafikia hadi waumini wa misikiti saba ya jimbo hilo.

Kwa upande wake, Sheikh wa Kata ya Kukirango, Juma Maharage, alisema imekuwa ni desturi ya Sagini kuwalika wananchi mbalimbali katika kushiriki kitoweo kwa pamoja.

Baadhi ya taasisi zilizofikiwa na kitoweo hicho ni shule za sekondari Kiagata, Bumangi, Chief Ihunyo, Chief Wanzagi, Mkono, shule ya mahitaji maalum Kiabakari, Chuo cha Victoria Nyabange, Musoma Utalii, Hope for Girls and Women Tanzania, Magereza na VETA Butiama.

Aidha, tukio hilo ni muendelezo wa majitoleo anayofanya Sagini katika jamii kila mwaka sio tu kwa Waislamu bali pia kwa Wakristo, ambapo ameendelea kuwagusa katika kusaidia ujenzi, kushiriki sikukuu zao na utoaji wa zaka mbalimbali.

Lengo kubwa la majitoleo hayo ya Sagini ni kuifanya jamii kuwa pamoja na kudumisha mshikamano uliojengwa toka zamani.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages