NEWS

Thursday, 28 May 2026

Madiwani Serengeti wampongeza Makuruma kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa



Mwenyekiti mpya wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma.

Na Godfrey Marwa
Serengeti
--------------------------------------------

Baraza la Madiwani la Halmashauri Wilaya ya Serengeti limempongeza Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Mara.

Madiwani wa baraza hilo walitoa pongezi hizo wakati wa kikao cha chao kilichofanyika wilayani hapa wiki iliyopita, huku wakimtaja Makuruma kama kiongozi imara na mwadilifu.

"Ninamfahamu ndugu yetu Makuruma, nimekuwa makamu wake kwa miaka mitano mfululizo. Hakika ALAT Mkoa wa Mara imepata mwenyekiti imara asiyeogopa.

"Makuruma ni muwazi, mkweli na mbunifu, na tuna imani ataingoza ALAT Mkoa wa Mara kwa mafanikio makubwa pia,” alisema Diwani wa Kata ya Kisangure, Samson Ryoba Wambura.

Madiwani wengine walimtaja mwenyekiti huyo mpya wa ALAT kama kiongozi mbunifu ambaye katika kipindi cha uongozi wake halmashauri hiyo imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato ya ndani.

Madiwani hao wa Chama tawala - CCM waliahidi kuendelea kumpa Makuruma ushirikiano wa dhati katika safari yake ya uenyekiti wa halmashauri hiyo na ALAT mkoa.

Machi 4, mwaka huu, Makuruma alishinda nafasi ya kiti cha ALAT Mkoa wa Mara katika uchaguzi ulioshuhudia ushindani mkali mjini Musoma, makao makuu ya mkoa huo.

Miongoni mwa majukumu ya ALAT ni kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha (value for money) na kila halmashauri inapata maendeleo bila kubaki nyuma.

Ni chombo ambacho huwakutanisha wenyeviti na wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa na madiwani wanaoteuliwa kuwa wajumbe wa jumuiya hiyo.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages