NEWS

Monday, 25 May 2026

TAKUKURU Mara yafanikisha urejeshwaji wa shilingi milioni 58 kwa mamlaka za serikali, watumishi wa umma



Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Mara, Mohamed Shariff, akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma.

Na Mwandishi wetu
Musoma
----------------

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imefanikisha urejeshwaji wa malipo ya shilingi milioni 58 kwa mamlaka mbalimbali za serikali na watumishi wa umma kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026 mkoani humo.

Hayo yalielezwa na kwenye taarifa ya utendaji kazi katika kipindi hicho iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Mara, Mohamed Shariff, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Musoma, wiki iliyopita.

Kwa mjibu wa Shariff, fedha hizo zimerejeshwa kupitia uzuiaji wa rushwa na uchambuzi wa kiutendaji kwenye taasisi mbalimbali.

Shariff alielezea kuwa katika tukio moja, walimu 118 wa shule za msingi na sekondari wilayani Butiama walikatwa shilingi zaidi ya milioni 10 kutoka kwenye nauli zao za likizo kinyume na taratibu, ambapo baadaye zilirejeshwa.

"Baada ya ufuatiliaji tulibaini fedha hizo zilitumika isivyo sahihi kuwalipa posho maofisa walioshughulikia malipo ya nauli kinyume cha sheria," alifafanua Shariff.

Katika sekta ya maji, alisema TAKUKURU imefanikisha kurejesha shilingi milioni 14.6 kwa mamlaka saba za huduma za maji ngazi ya jamii wilayani Musoma, baada ya kubainika udhaifu katika ukusanyaji wa madeni ya wateja yaliyodumu zaidi ya mwaka mmoja.

Kwa upande mwingine, alisema kijiji cha Seka katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kimepokea shilingi milioni 12.6 kutoka kampuni ya uchimbaji madini MMG kama fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), ambapo zilikuwa zikipitia halmashauri badala ya kuweka moja kwa moja kwenye kijiji kama ilivyo kwenye mkataba.

Vilevile, Mkuu huyo wa TAKUKURU alisema kijiji cha Nyanjage wilayani Rorya kimepokea shilingi milioni 9.6 kama mrabaha wa mchanga wa dhahabu baada ya kubainika dosari katika usimamizi wa mgodi ambapo fedha zilikuwa hazikabidhiwi kikamilifu kwa serikali ya kijiji hicho.

Aidha, Shariff alisema shilingi milioni 10 zilirejeshwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi baada ya kubainika upungufu kwenye ushughulikiaji wa faini za uvuvi haramu, ambapo washukiwa walishindwa kulipa kwa wakati hadi TAKUKURU ilipoingilia kati.

Alibainisha kuwa katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilifanikiwa pia kuwafikia wananchi zaidi ya 54,000 na kuwapa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa, ikilenga kusisistiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kupambana na kudhibiti vitendo hivyo kwa maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages