NEWS

Wednesday, 27 May 2026

UDSM wawatunuku TANESCO cheti cha sekta wezeshi maendeleo ya elimu jumuishi, ustawi wa wanafunzi




Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) limetambuliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kama miongoni mwa sekta wezeshi zinazochangia maendeleo ya elimu jumuishi na ustawi wa wanafunzi chuoni hapo.

Utambuzi huo umetolewa Mei 26, 2026, katika hafla maalum ya kuwatambua na kuwapongeza wadau wa maendeleo wa chuo hicho, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa UDSM na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema wadau mbalimbali wakiwemo TANESCO wana mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi.

“Tunapowasaidia wanafunzi hawa, hatuwafanyii fadhila. Tunathibitisha uwezo wao, utu wao na nafasi yao halali katika elimu ya juu,” amesema Dkt. Kikwete.

Aidha, ameshukuru wadau wote wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na chuo hicho katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wa TANESCO, cheti hicho cha utambuzi na pongezi kilipokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Irene Gowelle, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Lazaro Twange.

Dkt. Kikwete akimkabidhi Irene cheti hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO.

Utambuzi huo umetolewa ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wa TANESCO katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujisomea kwa wanafunzi na wakufunzi wenye changamoto mbalimbali za ulemavu na mahitaji maalum chuoni hapo.

Hafla hiyo ilibebwa na kaulimbiu isemayo “Kujenga Mazingira Jumuishi ya Kujifunzia kupitia Ushirikiano wa Kimkakati”, ikiwa na lengo la kuhamasisha ushirikiano kati ya taasisi, wadau wa maendeleo na jamii katika kuendeleza elimu jumuishi nchini.

Katika hafla hiyo pia, Dkt. Kikwete alizindua rasmi mbio za “UDSM Marathon 2026” zitakazofanyika Desemba 5, 2026, zikiwa na lengo la kukusanya rasilimali kwa ajili ya kusaidia elimu jumuishi, ustawi wa wanafunzi na programu za kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages