
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (wa nne kulia mbele), akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kiliniki ya Kusikiliza na Kushughulikia Malalamiko ya Wananchi kwa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------------
Tarime
----------------
Serikali wilayani Tarime imeipongeza kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick kwa kuanzisha kliniki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ikiwa ni mwendelezo wa kuimarisha zaidi mahusiano na jamii inayouzunguka.
Mwaka jana, kliniki hiyo ilisikiliza malalamiko na maoni mbalimbali ya wananchi katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo unaoendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Vijiji hivyo ni Mjini Kati, Nyangoto, Kewanja, Matongo, Nyabichune, Kerende, Nyakunguru, Komarera, Genkuru, Msege na Nyamwaga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo Mei 26, 2026 katika kijiji cha Mjini Kati kilichopo Nyamongo, Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza kama si kumaliza malalamiko na migogoro kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka.
“Niupongeze mgodi wa Barrick North Mara kwa kuanzisha kliniki hii, ni hatua kubwa. Ni matumiani yangu kuwa itapunguza malalamiko na migogoro. Ili kujenga jamii ya amani na utulivu lazima tusikilize na kutatua migogoro iliyopo,” alisema.

Meja Gowele akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kliniki hiyo.
Meja Gowele alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wanavijiji kujitokeza kuwasilisha malalamiko yao kwenye kliniki hiyo ili yapatiwe ufumbuzi kwa maendeleo na ustawi wa pande zote mbili.
Aidha, aliitaka kamati ya kliniki hiyo na viongozi wa vijiji kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati kuhusu mikutano ya kusikiliza na kupokea malalamiko yao itakayofanyika katika kila kijiji.
“Nimezindua rasmi kliniki hii, ipite kila kijiji na kusikiliza kila mwananchi mwenye malalamiko bila ubaguzi wala upendeleo,” Meja Gowele alisisitiza.
Sehemu ya wananchi kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi huo wakiwa kwenye uzinduzi wa klinini hiyo.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya aliendelea kutoa msisitizo kwa watu waliopo ndani ya eneo la leseni ya Barrick North Mara kutii sheria bila shuruti na kuondoka ili kutokwamisha shughuli za mgodi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika mgodi wa Barrick North Mara, Bogomba Rashid, alisema hatua hiyo ya kusikiliza na kutatua migogoro itasaidia pia kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Mwenyekiti wa CDC na Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Rashid, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kliniki hiyo.
Viongozi wengine wa kijamii na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kliniki hiyo walisema itasaidia kupunguza malalamiko yanayohusiana na shughuli za mgodi huo na hivyo kuimarisha zaidi mahusiano baina ya pande zote mbili [jamii na mgodi].
Kikundi cha ngoma ya asili ya kabila la Wakurya ikitoa burudani katika hafla ya uzinduzi huo.
“Tunawapongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa hili walilofanya la kuzindua hii kliniki, limekuja wakati mwafaka,” alisema Eliza Malembera, mmoja wa madiwani wa viti maalum kutoka kata zinazozunguka mgodi huo.
Meneja wa Idara ya Mahusiano ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo.
DC ataka ujenzi miradi ya kimkakati ya CSR uanze mara moja
Mkuu wa Wilaya pia alielekeza mgodi kuhakikisha miradi ya kimkakati inayogharimiwa na fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) inatekelezwa kwa wakati bila kucheleweshwa kwa visingizio vya michakato.
Miradi hiyo ni ujenzi wa Soko la Dhahabu katika mji mdogo wa Nyamongo na Stendi ya Mabasi katika senta ya biashara ya Nyamwaga.
“Lazima hii miradi itekelezwe kwa wakati, jengo hili [Soko la Dhahabu] likisimama vijana wataanza kupata ajira. Nisingependa kuona michakato inachelewa.
Meja Gowele (aliyevaa suti na shati jeupe) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kijamii, Mgodi wa Barrick North Mara na asasi za kiraia.
Akizungumzia miradi ya kimkakati ya ujenzi wa Soko la Dhahabu Nyamongo na Stendi ya Mabasi Nyamwaga, Meneja alisema iko kwenye hatua za manunuzi huku ikisubiri idhini ya Tume ya Madini ili kuendelea na zabuni za wakandarasi.
“Mradi wa soko la dhahabu ambao ni wa kisasa utabadilisha mandhari ya hapa [Nyamongo],” alisema Uhadi.
Kuhusu miradi ya kijamii mipya inayotekelezwa pia kupitia mpango wa CSR, Uhadi alisema hadi sasa miradi 70 kati ya 103 imekamilika kwa asilimia 100 na 33 iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.





No comments:
Post a Comment